Wednesday , 22nd Feb , 2017

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai Mhe. Freeman Mbowe amefunguka na kusema kuwa anahitaji nchi irejee katika misingi ya utawala wa katiba, sheria na utaratibu.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Mhe. Freeman Mbowe kupitia mitandao ya kijamii amesema kutokana na jina lake kuhusishwa na tuhuma za dawa za kulevya bila ushahidi katika hilo ni lazima adai haki yake kwa kuchafuliwa jina lake.

"Mimi ni kiongozi wa watu, ni Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ni Baba mwenye familia na watoto ni Mbunge wa jimbo la Hai naaminika na wananchi na mahusiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, napokuwa nasikia nimetuhumiwa kwa tuhuma za dawa ya kulevya ambazo hazina ushahidi, hazina msingi ni jambo baya sana ni 'character assassination'. Nina mipango wa kudai fidia kwa kuchafuliwa jina, hilo liko wazi nilisema toka siku ya kwanza kwa hiyo mpango huo lazima tutautekeleza." alimaliza Freema Mbowe.

Mbowe amezungumza haya ikiwa ni siku moja baada ya mahakama kulizuia jeshi la polisi kumkamata hadi hapo kesi yake ya kikatiba itakapoamuliwa.

Freeman Mbowe akizungumza na wanahabari je ya mahakama

Mbali na hilo Freema Mbowe amesema kwa sasa anapambana na dola, anapambana na serikali vyombo vya usalama pamoja na mkuu wa mkoa lakini anatambua kuna watu wengi wanapata shida kama yeye lakini hawana uwezo wa kudai haki zao hivyo yeye mapambano yake ni ni katika kupigania haki katika taifa ili taifa liendeshwe kwa mujibu wa katiba, sheria na utaratibu wa nchi na si vinginevyo.

"Viongozi wa Kiserikali au viongozi wenye mamlaka juu ya watu wengine wasijione wao wana haki ya kutenda mambo kinyume cha katiba, kinyume cha taratibu hata kama jambo wanalotaka kufanya lina njia njema, lazima yapitie katika mfumo unaokubalika wa kisheria. Ninapoidai haki hii siyo kwamba naipigania haki mimi kama Mbowe hapana, napigania haki katika taifa, taifa liendeshwe kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu za nchi" alisisitiza Mbowe