Mshambuliaji Mtanzania Mbwana Samatta[jezi ya Bluu] akiwajibika katika klabu yake ya Genk ya Ubelgiji.
Jamal Kisongo ambaye ni Meneja na Mlezi wa Samatta, amesema hakuna lolote kuhusiana na hilo na Samatta anaendelea na maandalizi katika kikosi chake cha KRC Genk kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
“Nimesikia pia, kuna watu kadhaa wameniuliza pia. Lakini ukweli ni hivi, Mbwana anaendelea na maandalizi ya Ligi Kuu ya Ubelgiji na timu yake ya sasa Genk," alisema Kisongo na kuongeza “Hakuna lolote kuhusiana na hao Roma hadi sasa labda kama litakuja baadaye. Mawakala wake wote wanalijua hilo".
Kuanzia leo majira ya asubuhi, kulienea taarifa za AS Roma ya Italia imekuwa kwenye mazungumzo Genk juu ya uwezekano wa kumnasa Samatta ambaye ni nahodha wa taifa Stars, na hasa katika mitandano ya kijamii habari hizo zimekuwa zikisambaa kwa kasi kubwa nakuzua maswali mengi na wengi wakipongeza kwa hatua za haraka za mchezaji huyo Mtanzania.
Nyota ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania imeendelea kung'ara katika klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji baada ya kufunga mabao mfululizo ndani ya siku mbili katika mechi za kirafiki za kujiandaa na msimu mpya.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC, juzi alifunga bao moja katika ushindi wa 3-0 juzi dhidi ya ESK Leopoldsburg nyumbani.
Samatta alifunga bao la kwanza dakika ya 20 Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk, wakati mabao mengine yalifungwa na Karelis dakika ya 29 na Walsh dakika ya 66.
Kabla ya hapo, Samatta alifunga pia katika ushindi wa 5-0 kwenye mchezo mwingine wa kirafiki wiki ugenini dhidi ya Bocholt Julai 1.
Samatta alifunga dakika ya 68 likiwa bao la nne, wakati mabao mengine yamefungwa na Kebano dakika ya 15, de Camargo dakika ya 45 yote kwa penalti, Trossard dakika ya 47 na Heynen dakika ya 88.
Kabla ya mechi hiyo ya Julai 1, Samatta aliichezea pia Genk katika mchezo wa kirafiki Juni 25, ikishinda 7-1 dhidi ya Unity Termien.
Lakini siku hiyo, Samatta hakufunga na mabao ya timu yake yalifungwa na de Camargo, Dewaest, Kebano, Sabak, Van Zeir, Karelis na Pozuelo huku la wapinzani wao likifungwa na Baur.
Genk watashuka tena dimbani Julai 7 kumenyana na Lommel, Julai 9 na Lierse na Julai 17 na FC Eindhoven.