Saturday , 25th Jun , 2016

Hatua ya mtoano ya kombe la Mataifa ya Ulaya Euro 2016 imeenza huku ikishuhudiwa timu ya Poland ikitangulia kutinga robo fainali ya michuanho hiyo nakuiondosha mashindanoni timu ngumu ya taifa ya Uswizi kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Wachezaji wa timu ya Taifa ya Poland wakishangilia baada ya kutinga robo fainali ya Euro 2016.

Mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya 16 bora ya michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2016 imenaza katika mji wa Saint-Etienne ukichezwa jioni ya leo nakudumu kwa dakika 120 na baada ya kwenda sare ya bao 1-1.

Poland walitinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo wakitokea kundi C nafasi ya pili nyuma ya vinara wa kundi hilo Ujerumani huku Uswizi wao wakifika hatua hiyo wakiwa nafasi ya pili kutoka kundi A nyuma ya wenyeji Ufaransa.

Poland inafuzu hatua hiyo ya robo fainali ya michuao hiyo ya Ubingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo baada ya shujaa wao mchezaji Jakub Blaszczykowski kufunga penati muhimu ya mwisho katika ushindi huo wa mikwaju ya penati 5-4 dhidi ya Uswizi.

Mchezaji mpya wa klabu ya Arsenal Granit Xhaka alikuwa na huzuni kubwa baada ya kushuhudia penati yake pekee ikiota mbawa katika mchezo huo mjini Saint-Etienne.

Na ilikuwa jioni yenye furaha na hisia ya aina yake kwa mchezaji wa Stoke City Xherdan Shaqiri ambaye alifunga goli bora la mashindano hayo kwa staili ya akrobatiki lakini halikuisaidia timu yake kubaki mashindanoni baada ya kutupwa nje kwa mikwaju ya penati.

Mchezo huo wa kwanza wa hatua hiyo ya 16 ulitabiliwa kuwa ungeishia kwa suluhu ya 0-0 na kwenda katika hatua ya mikwaju ya penati hasa kufuatia rekodi ya timu hizo, ambapo Poland wao hawajawahi kufungwa goli katika hatua ya makundi huku Uswizi ikiruhusu goli moja tu tena la mkwaju wa penati.

Katika michezo mingine ya hatua hiyo iliyopigwa leo (Jumamosi) imeshuhudia Ureno ikifuzu Robo Fainali kwa bao pekee la dakika ya 117 dhidi ya Croatia, lililofungwa na Ricardo Quaresma na Wales ikiifunga Ireland ya Kaskazini ka bao pekee la kujifunga kutoka kwa Gareth McAuley dakika ya 75.