
Moja ya picha iliyovuja mitandaoni ikionyesha kiungo wa Mtibwa Sugar Mohammed Ibrahim "MO" akisaini mkataba wa kuitumikia klabu ya Simba kwa msimu ujao, na kushoto ni Rais wa Simba Evans Aveva akishuhudia kwa umakini
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Simba Zakaria Hans Poppe, ameshusha lawama kwa Wakala wa wachezaji, Jamal Kisongo, kwa kuvujisha picha za usajili wa mchezaji anayemmiliki ambaye amesaini klabu hiyo, hivi karibuni.
Poppe, amesema kamati yake ilikubaliana zoezi hilo lifanyike kimya kimya na likikamilika ndiyo litangazwe, ili kuondoa wavurugaji wanao iharibia klabu hiyo.
Picha iliyovuja kwenye vyombo vya habari ni ya kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohamed Ibrahim 'Mo', aliyeonekana akisaini karatasi za wekundu wa Msimbazi mbele ya Rais wa klabu hiyo Evans Aveva mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo awali Kisongo aliiomba picha hizo kwa kumbukumbu zake laini imekuwa sivyo.
Aidha kwa upande mwingine Poppe amesema hadi kufikia mwishoni mwa wiki hii, zoezi la wachezaji wa ndani litakuwa limekamilika na litakalofuata ni la wachezaji wa kimataifa ambao wanafanya nao mazungumzo hivi sasa.