Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya ngumi wakifanya mazoezi.
Baada ya kukosa kocha mwenye nyota tatu hatimaye Shirikisho la ngumi nchini Tanzania BFT limefanikiwa kukamilisha makubaliano na kocha mwenye sifa za hizo ambaye ataungana na timu ya taifa ya ngumi wakati wowote kwaajili ya maandalizi ya michuano ya kufuzu Olimpiki na baadae mashindano yenyewe.
Rais wa BFT Muta Rwakatale amesema wamempata kocha Musa Benjamini Oyandi kutoka nchini Kenya mwenye hadhi ya nyota tatu ambayo ni moja ya sifa kubwa ya kocha kumwezesha kupandisha bondia ulingoni katika michuano ya Olimpiki.
Aidha Muta ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kawe jijini Dar es Salaam amesema ujio wa kocha huyo utategemea na ni lini kikosi cha timu ya taifa ya ngumi kitaingia kambini kwaajili ya maandalizi ya michuano ya mwisho ya mchujo otakayofanyika nchini Venezuela mapema mwezi Julai mwaka huu ndipo watamwita kocha huyo kuanza kibarua hicho.
Muta amesema wameuangalia na kuusoma kwa umakini mkubwa wasifu [cv] wa kocha huyo na uzoefu alionao ndiyo kitu kikubwa walichokiangalia na kuamua kufanya naye mazungumzo kocha huyo ambaye anauzowefu wa kutosha wa kupeleka mabondia wengi wa kimataifa katika michuano mikubwa duniani.
Akimalizia Muta amesema kwa sasa wanasubiri wachezaji waajiliwa wa vyombo vya usalama [taasisi za majeshi] ambao bado hawajapata ruhusa kutoka kwa waajili wao ili waruhusiwe na kukamilisha kikosi cha timu ya taifa tayari kwa maandalizi ya kuelekea mashindano hayo ya mchujo yatakayofanyka nchini Venezuela.
Pia ametoa wito kwa Watanzania kuisaidia timu hiyo ili iweze kujiandaa kikamilifu na kuipeperusha vema bendera ya Taifa katika medani ya kimataifa na akakumbusha kuwa katika michezo yote kwa miaka ya hivi karibuni ni mchezo wa masumbwi pekee umekuwa ikishuhudiwa wanamasumbwi wakiitangaza nchi vizuri kwa kutwaa mikanda ya ubingwa wa dunia na kimataifa hivyo wanapaswa kuungwa mkono kwa hali na mali badala ya kuliachia shirikisho la mchezo huo pekee.