
Serikali imesema haitamvumilia mfanyakazi yeyote wa mizani atakaebainika anajihusisha na vitendo vya rushwa ili kuruhusu mizigo kupita bila ya kupimwa katika vituo vya mizani.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Uajenzi) Mhandisi Joseph Nyamhanga wakati alipokagua huduma za upimaji uzito wa magari katika Mzani wa Njuki Mkoani Singida na kubainisha hatua zitakazochukuliwa kuwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wale watakaobainika.
Aidha, amewataka madereva wa magari na abiria nchini kushirikiana na wizara hiyo kutoa taarifa za wafanyakazi wa mizani wanaowaomba rushwa ili kuweza kuondoa kero kwa wananchi wanaotumia huduma za mizani na kuwaomba madereva hao kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari ili kuepusha uharibifu wa barabara.