Friday , 3rd Jun , 2016

Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi kimeiva tayari kuwavaa Mafarao wa Misri hapo kesho huku nahodha Mbwana Samatta akiwataka mashabiki kujitokeza uwanjani hapo kesho kutoa hamasa.

Nahodha wa Stars Mbwana Samatta [kushoto] akiwa na kocha wake Boniface Mkwasa.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba kikosi chake kimekamilia kwa wachezaji wote kuwa katika ari ya mchezo na kwamba hakuna majeruhi yanayoweza kumzuia hata mmoja wa wachezaji wake kuitumikia timu yake hapo kesho.

Stars yenye alama moja ikiwa na mchezo mmoja zaidi mkononi dhidi ya Nigeria utakaopigwa Septemba mwaka huu inaingia katika mchezo huo wa mwisho kwa Wamisri ambao wana alama saba ikihitaji kupata matokeo ya ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa AFCON.

Mkwasa ambaye enzi za uchezaji wake alijulikana kama Masta amesema kwa mazoezi waliyofanya anaimani kubwa ya kuibuka na ushindi hapo kesho katika mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam na kimsingi kila mchezaji anatambua deni walilonalo kwa Watanzania.

Kwaupande wake nahodha wa Taifa Stars Mbwana Ally Samatta ambaye anakipiga katika timu ya KRC Genk inayoshiriki ligi kuu ya Ubelgiji amesema wanaiheshimu Misri lakini lengo lao ni kuibuka na ushindi japo mchezo utakuwa mgumu.

Nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amewakaribisha Watanzania kuishangilia timu ya soka ya Tanzania - Taifa Stars ambayo kesho Juni 4, 2014 itacheza dhidi ya Misri katika mchezo wa kuwania nafasi kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mwaka 2017 huko Gabon.

Samatta amesema mchezo huo ni muhimu sana kwa Watanzania katika kuhakikisha wanabadilisha upepo wa soka kwakuwachapa Mafarao hao na kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa fainali hizo na pia kuipandisha nchi katika viwango vya ubora wa soka barani Afrika [CAF] na [FIFA].