Viongozi na wanariadha wa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja ndani ya uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Tanzania inataraji kuwa mwenyeji wa michuano mingine ya vijana kwa nchi za Afrika Mashariki baada ya kamati ya utendaji ya shirikisho la riadha kwa nchi za Afrika Mashariki EAAF kukubaliana hapo jana kwa kauli moja kuipa uenyeji Tanzania kuandaa michuano ya vijana safari hii ikiwa ya umri wa miaka chini ya 18.
Taarifa hiyo imetolewa na makamu wa kwanza wa Rais wa Riadha Tanzania RT William Kalaghe wakati akizungumzia changamoto na mafanikio ya mashindano ya riadha ya vijana chini ya miaka 20 kwa nchi za Afrika Mashariki yajulikanayo kama Eastern Zone Africans Althletics Championship 2016 yaliyofanyika jijini Dar es salaam kwa siku mbili kuanzia Aprili 29 na kumalizika Aprili 30.
Kalaghe amesema pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa namna moja au nyingine katika mashindano hayo ya U20 maandalizi bora katika maeneo yote muhimu ya mashindano pamoja na moyo wa ushirikiano sambamba na miundombinu bora ya mashindano ikiwemo uwanja wenye hadhi ya kimataifa ni moja ya sababu ambayo imepelekea umoja wa riadha kwa nchi za Afrika Mashariki kuipa tena uwenyeji Tanzania kuandaa michuano mingine ya vijana chini ya miaka 18.
Katika mashindano hayo ya mwaka huu Kenya imetawala kwa kiasi kikubwa na kuzishinda nchi nyingine.
Akimalizia Kalaghe ametowa wito kwa wadau wa michezo makampuni na hasa serikali kusaidia kwa hali na mali maandalizi, kwanza kwa timu ya taifa itakayoshiriki michuano hiyo na nyingine iweze kufanya vema lakini pia kwa kamati ya maandalizi ili iweze kufanya maandalizi bora zaidi yanayoendana na mashindano husika yenye hadhi ya kimataifa.