Friday , 25th Mar , 2016

Bondia chipukizi ambaye anasifika kwa uwezo mkubwa wa kusukuma masumbwi mazito kwa wapinzani wake Ibrahim Tamba wa Dar es salaam ametamba kumshushia kipigo kizito mpinzani wake Said Mbelwa ambaye watavaana kuwania mkanda wa taifa wa uzito wa juu.

Mabondia Ibrahim Tambwe kushoto na Said Mbelwa kulia wakitunishiana misuli.

Mabondia wa Tanzania Ibrahim Tamba wa Dar es Salaam na Said Mbelwa wa Tanga hii leo wamepima uzito na afya zao tayari kwa mpambano wao wa kimataifa wakuwania ubingwa wa taifa mkanda wa PST uzito wa Light Heavy utakaopigwa kesho jijini Dar es Salaam.

Mabondia hao wanakutana kila mmoja akiwa na dhamira ya kutetea mkoa wake na kubwa ikiwa kuweka rekodi kwa kutwaa mkanda huo japo mashabiki wengi wametabiri ugumu wa mchezo huo kutokana na rekodi za mabondia hao lakini pia uwezo binafsi wa kila mmoja wao katika mbinu za kiufundi na kiupiganaji na uzoefu wa mapigano mengi ya kimataifa.

Wakizungumza baada ya zoezi la upimaji uzito na afya mabondia hao wakiwa wameambatana na mashabiki wao lukuki kila mmoja ametamba kumtwanga mwenzake na kuibuka na ushindi hiyo kesho jambo ambalo limeongeza msisimko mkubwa kuelekea mpambano huo wa Machi 26.

Kwa upande wao chama cha ngumi za kulipwa nchini Tanzania PST ambao ndiyo wasimamizi wa mpambano huo kupitia kwa rais wake Emmanuel Mlundwa amethibitisha zoezi la vipimo kwenda sawa sawa kwa mabondia hao watakaopigania uzito wa juu kulingana kwa kilo lakini pia kwa upande wa afya vipimo vikionesha mabondia hao wako fiti na wameruhusiwa kisheria kwa mujibu wa ataratibu za masumbwi kushuka ulingoni kuwania mkanda huo.