Tuesday , 26th Jan , 2016

Mkutano wa pili wa Bunge la 11 umeanza hii leo mjini Dodoma pamoja na shughuli nyingine wabunge watajadili mpango wa maendeleo awamu ya pili na hotuba aliyoitoa Rais Dkt. Magufuli huku mjadala wa kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar ukitarajiwa kuibuka.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai

Mkutano huo umeanza kwa kiapo cha uaminifu kwa wabunge 11 ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na Rais pamoja na kipindi cha maswali na majibu kwa wizara tofauti za serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu ratiba ya mkutano huo wa bunge mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano Bungeni Owen Mwandumbya amesema mkutano huo ulioanza utamalizika Februari 05 mwaka huu.

Aidha mkuu huyo wa kitengo cha habari ameongeza kuwa katika mkutano huo jumla ya maswali ya msingi ya kawaida 125 yanategemewa kuulizwa na kujibiwa huku maswali ya msingi 16 yakielekezwa kwa Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa shughuli zitakazoendeshwa leo ni pamoja na uchaguzi wa wenyeviti watatu wa bunge na ambapo juzi kamati ya uongozi ilipendekeza majina ya wabunge watatu ambao ni Najma Giga, Andrew Chenge na Marry Mwanjelwa kuwania uenyekiti huo.