URA ya Uganda Mabingwa wa Mapinduzi Cup wakisherehekea ushindi
Ushindi huo ambao unakwenda sambamba na kitita cha Sh. Milioni 10, unaifanya URA iwe timu ya pili ya Uganda kutwaa taji hilo, baada ya KCCA mwaka juzi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nassor, hadi mapumziko, URA walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Julius Ntambi kwa kichwa, akimalizia krosi ya Villa Oromchani kutoka upande wa kushoto.
URA walikaribia kupata bao la pili dakika ya 37 baada ya Elkannah Nkugwa kupiga nje na kupoteza pasi ya Moor Semakula.
Kwa ujumla, URA ilitawala mchezo na kuishika Mtibwa Sugar, ambayo safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Hussein Javu anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC, iliishindwa kupasua ukuta wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda.
Kipindi cha pili cha mchezo Mtibwa Sugar iliyochini ya kocha Mecky Mexime ilijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la kusawazisha, lakini wakasahau kuongeza umakini wa kujilinda, hivyo kuwapa fursa URA kupata mabao mawili zaidi.
Kpindi cha pili cha mchezo Peter Lwasa aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Villa Oromchani, aliifungia URA mabao mawili ndani ya dakika tatu ambapo bao la pili lilifungwa dakika ya 85 baada ya beki Dickson Daud kujichanganya na kuugawa mpira huku bao la tatu likipatkana dakika ya 88 akimalizia pasi ya Julius Ntambi.
Jaffar Salum aliyeingia kuchukua nafasi ya Hussein Javu mwishoni mwa kipindi cha pili, aliifungia bao la kufutia machozi Mtibwa Sugar dakika ya 90, baada ya kumlamba chenga Jimmy Kulaba.
Pamoja na kutwaa ubingwa, URA pia imetoa mfungaji bora, ambaye ni Peter Lwasa aliyemaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Villa Oramchani wa URA pia, mabao mawili sawa na Awadh Juma wa Simba SC, Donald Ngoma wa Yanga SC, Mohammed Abdallah wa JKU na Kipre Tchetche wa Azam FC.
Mtibwa Sugar wamepatiwa Sh. Milioni 5 kwa kushika nafasi ya pili.
Kikosi cha URA FC kilikuwa; Brian Bwete, Simon Massa, Alan Munaaba, Jimmy Kulaba, Sam Senkoom, Oscar Agaba, Julius Ntambi, Said Kyeyune, Moor Semakula/Shafiq Kagimu dk48, Villa Oramuchani/Peter Lwasa dk53 na Elkannah Nkugwa/Sam Sekito dk74.
Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Ally Shomary, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Daudi, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Mohammed Ibrahim, Muzammil Yassin, Hussein Javu/Jaffar Salum dk81, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ na Shiza Kichuya/Said Bahanuzi dk69.


