Kamanda Mpinga ameyasema hayo leo katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mkoani Ubungo jijini Dar es salaam baada ya kituo hicho kufurika watu wengi kuliko uwezo wa magari yaliyopo huku wengine wakiwa na tiketi feki za kusafiria.
''Ni wajibu wa kila abiria kuhakikisha anakua makini na maisha yake ,kuna wengine wamekata tiketi feki kutoka kwa madalali na wanapofika kwenye mabasi husika wanaambiwa hawatambuliki jambo ambalo linaleta usumbufu mkubwa,hivyo ni wajibu wa kila msafiri kuhakikisha anakata tiketi katika ofisi ya gari husika ili kuepusha lawama na usumbufu usio wa lazima'' amesisitiza kamanda Mpinga.
Kamanda mpinga amesema kuwa kwa siku mabasi yanayoenda mikoani msimu huu wa sikukuu na nchi jirani ni zaidi ya 528 na kubeba abiria elfu ishirini na tatu lakini bado abiria ni wengi sana ambao wamebaki bila usafiri na bado wapo katika kituo hicho.
Kutokana na adha ya usafiri kituoni hapo Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa Nchi kavu na majini (SUMATRA) imetoa kibali kwa mabasi maalumu kufanya safari msimu huu hasa katika mikoa ya kaskazini ili kusaidia abiria kuweza kusafiri.
Aidha Kamanda Mpinga amewataka wasafiri kutambua kuwa usalama wao na mali zao upo mikononi mwao wanapokua safarini na kuwahimiza kutoa taarifa pindi wanapoona dereva anakimbia mwendo usio salama au kama anapita magari mengine bila tahadhari na wasisite kuwatafuta jeshi la polisi kwa simu namba 0682887722 ili kupata usaidizi wa haraka.
Hata hivyo kamanda mpinga amewaasa abiria kuhakikisha waatoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la polisi wanaokua katika vituo mbalimbali barabarani na pia wakiona dereva anakimbiza gari kwa mwendo hatarishi wapaze sauti wamtake aendeshe kwa mwendo halali.