Tuesday , 17th Nov , 2015

Msanii Profesa Jay ambaye pia ni mbunge mteule wa jimbo la Mikumi, amesema pamoja na kuingia bungeni humo kuwatumikia wananchi, hatoacha kuwatetea wasanii kwani pia yeye ni mmoja wapo.

Profesa Jay ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na moja ya kituo cha televisheni, na kueleza kuwa kama msanii anajua changamoto zao wanazopitia, hivyo hatosita kufanya hivyo, kwani pamoja na kuingia bungeni ataendelea kufanya sanaa, na anajua changamoto wanazokabiliana nazo wasanii.

"Ukiwa mtu unayefuatilia muziki utaona harakati zangu zilianzia huko, sanaa ni kipaji imenisaidia kupaza sauti na nitapaza sauti zaidi, tumepiga kelele sana lakini hakuna mafanikio, nadhani sasa ndiyo muda muafaka wa kupaza sauti zaidi ili isikike, na kama unavyojua platform ya muziki inafika haraka sana, hivyo nitajitahidi kupaza sauti zaidi ili matatizo ya wasanii yapate ufumbuzi", alisema Profesa Jay.

Profesa Jay aliendelea kwa kusema kuwa ingawa baadhi ya viongozi waliotangulia bungeni hapo walijaribu kuligusia suala la wasanii, lakini sauti yao haikufika popote kutokana na changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo, hivyo amewataka wasanii kuwa na umoja thabiti ili kuweza kufanikisha hilo.

"Ni kweli viongozi wengi waliotangulia walikuwa wanakatishwa tamaa kila wanapotaka kuingilia sanaa, hatutaweza kuendeleza sanaa yetu kama hatutakuwa na umoja wa wasanii, cha msingi ni kuwaweka wasanii pamoja, tuunganishe wasanii tupaze sauti, tukipaza sauti kwa pamoja na umoja itasaidia", alisema Profesa Jay.

Msanii huyo ambaye alikuwa anafanya kampeni zake jimboni humo, amesema hakuchukizwa na kitendo cha wasanii wa chama kingine kufanya kampeni za kumpinga jimboni hapa, kwani walikuwa kazini hivyo atakapoanza kutetea wasanii, nao watakuwa miongoni mwao huku bado akisisitiza suala la umoja.

"Sikutengeneza gape kati wasanii wakongwe na chipukizi, najua changamoto zao, tunahitaji sana umoja wa wasanii, kipindi mi nafanya kampeni kuna wasanii nao walikuwa majukwaani wanapinga kampeni zangu, ile sio tatizo wasanii kuperfom jukwaani kunipinga, nitaendelea kuwapigania kwa nguvu zote, watakapoamua kukaa pamoja na kupaza sauti, tutafanikiwa kwa pamoja, alisema Profesa Jay.