Thursday , 1st Oct , 2015

Vijana wametakiwa kujitambua na kuelimisha wengine ambao hawana elimu, ili waweze kutambua wanatoka wapi na wanakwenda wapi, pamoja na kutambua rasilimali za nchi zilizopo na zinatumikaje.

Wito huo umetolewa na Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Bwana Michael bante, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Supermix kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kwamba vijana wengi hawajitambui na ndio maana hawajui rasilimali za nchi zinatumikaje, na kuendekeza starehe ambazo zinawarudisha nyuma kimaendeleo.

“Lazima muunde chama cha umoja wa vijana wanaojitambua, wale wanaojitambua waweze kuwaamsha wasiojitambua, wajue tunapokwenda na tunapotoka, wajue rasilimali zetu za nchi yetu, vijana lazima watambue rasilimali zao ni nani anazitumia, saa hizi rasilimali zenu wanazitumia wazee kwa nini wakati wao jua limezama?”, alisema Bante.

Pia Bante amesema kitendo cha vijana wengi kupenda starehe, kimewafanya watu wenye fedha kuwawekea miundo mbinu ya starehe ili kuwapumbaza mawazo yao, na kutohoji kuhusu rasilimali za taifa.

“Viongozi wameshagundua udhaifu wa vijana kwamba wanapenda starehe, kwa hiyo wananwaongezea kumbi za muziki, hizi kumbi za muziki zinajengwa na mafisadi, ni sa gharama kubwa, kumbi ukiingia kama uko marekani, club zimekuwa nyingi, zile kumbi mmewekewa nyie muongeze upumbavu na ujinga”, alisema Bante.

Pamoja na hayo Bante amesema Tanzania ina rasilimali nyingi lakini wananchi wake wanabaki kuwa masikini, kitendo kilichowapelekea vijana wengi kukata tamaa na serikali yao, na kutaka kubadilisha mfumo uliopo wakiamini watatatua changamoto za kiuchumi zilizopo.

Kwa upande mwengine Bwana Bante ameitaka serikali ijayo kufufua viwanda ili waweze kuajiri vijana ambao ni wazawa wa Tanzania, ili kuweza kutatua tatizo la ajira linaloikabili nchi, na kuondoa watu wageni waliowekwa kwenye sekta mbali mbali.

“Serikali ifufue viwanda, sasa hivi viwanda vingi ukienda wahindi, tuhakikishe wazawa watanzania wanapata kazi, sasa hivi watoto wetu wenye masters, Phd ni wengi, hivyo kwanza wapewe vijana watanzania, akihitajika mtu mwenye ujuzi fulani na watoto wetu hana, ndipo tuajiri kutoka nchi zingine tena tunazitaja iwe Kenya, uganda au wapi, ila kutoka Afrika”, alisema Bante.