Saturday , 19th Mar , 2016

Ligi kuu ya soka Tanzania bara ambayo inaendelea hivi sasa ikielekea ukingoni imekuwa na rekodi mbaya kwa washambuliaji wazawa kwani wamekuwa hawaonekani kuwa washindani katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora wa ligi hiyo.

Mshambuliaji hatari wa Tanzania Prisons Mohamed Mkopi pichani kushoto mwenye mpira.

Mshambuliaji hatari wa maafande wa Magereza kutoka jijini Mbeya timu ya Tanzania Prisons Mohamed Mkopi amesema washambuliaji wazawa hasa wanaoshiriki katika michuano ya ligi kuu Tanzania bara wameonekana kushindwa kushindana na washambuliaji wakigeni ni kutokana na baadhi ya washambuliaji wageni kuwezeshwa ama kurahisishiwa kazi na vilabu vyao.

Mkopi ambaye ni mchezaji bora wa mwezi wa pili amesema jambo lingine pia ni kwa washambuliaji wazawa wenyewe kutojitambua na hivyo kutoa mwanya na nafasi kwa washambuliaji wakigeni kuweza kuibuka na taji hilo kwa kuwa wao wanakuwa wakicheza kwa malengo ya kufikia hatua hiyo.

Pamoja na mambo hayo Mkopi pia amesema mifumo ya uchezaji nayo huwa ni moja ya sababu za wazawa kushindwa kufanya kile ambacho wengi wanakitarajia hasa katika suala la ufungaji akimtolea mfano, Mshambuliaji mzawa wa Yanga Simon Msuva ambaye mwaka jana aliibuka mfungaji bora lakini mwaka huu ameshindwa kabisa kutokeza hata katika wale wafungaji bora watano wanaoongoza katika ufungaji.

Mpaka sasa katika orodha ya tano bora ya washambuliaji wanaoongoza kwa ufungaji ligi kuu bara ikiwa imebakiza raundi saba washambuliaji wazawa bado wameonekana kuachwa kwa mbali na washambuliaji wa kigeni wanaoongozwa kwa sasa wakiongozwa na Mganda Hamis Kiiza wa Simba mwenye mabao 18, akifuatiwa na Mrundi Amis Tambwe wa Yanga mwenye mabao 17 huku Mzimbabwe Donald Ngoma wa Yanga akifuatia akiwa na mabao 13 na nafasi ya nne na tano wako wazawa Jeremiah Juma Mgunda wa Tanzania Prisons mwenye mabao 11 na anayekamilisha orodha ya tano bora ni mshambuliaji Elius Maguli wa Stand United mwenye mabao 10.

Kutokana na hali hiyo na kwa michezo iliyosalia Mkopi ambaye jumapili hii ataiongoza Tanzania Prisons katika mchezo wa ugenini dhidi ya Afrikan Sports amesema ni wazi kuwa washambuliaji wazawa wanakazi kubwa ya kufanya ili kuweza kutwaa kiatu cha ufungaji bora msimu huu ambao utamalizika mapema mwezi Mei mwaka huu.