Thursday , 24th Mar , 2016

Kufuatia ushindi wa kwanza wa ugenini chini ya kocha Mzawa Charles Boniface Mkwasa mbele ya timu ngumu ya Chad pongezi nyingi zinamiminika kwa timu ya taifa stars na benchi la ufundi la timu hiyo kwa mafanikio waliyopata na kufufua matumaini AFCON.

Nahodha wa stars Mbwana Ally Samata akiambaambaa na mpira jana wakati akiiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza dhidi ya Chad.

Wadau wa michezo nchini wameipongeza timu ya taifa ya Tanzania Taifa stars kwa kupata ushindi wa kwanza ugenini chini ya kocha Mzalendo Charles Boniface Mkwasa wakiwataka wachezaji kukaza buti na kushinda mchezo wa marudiano utakaopigwa siku ya jumatatu Machi 28 mwaka huu katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Wadau hao pamoja na pongezi zao kwa Stars ambayo inarejea nyumbani usiku wa kuamkia kesho baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya wenyeji Chad, bao lililofungwa na nahodha Mbwana Samatta wametoa wito kwa TFF kuhakikisha wanapunguza viingilio ili mashabiki wengi wakaipe sapoti timu hiyo.

Kwa upande mwingine pamoja ushindi wa bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya Chad, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema ilikuwa mechi ngumu sana kwao.

Mkwasa amesema vijana wake wamejituma vilivyo hadi kupata ushindi huo kwa kuwa walicheza katika mazingira magumu na hali ya hewa isiyokuwa rafiki kwao.

Aidha Mkwasa amesema ilikuwa ngumu sana hasa kutokana na hali ya hewa. "Hali ya hewa ilikuwa mbaya kabisa lakini vijana wangu walijituma na wanastahili pongezi kabisa," alisema.

Stars sasa imefikisha pointi 4 baada ya kucheza mechi tatu, ikiwa imepoteza moja, sare moja na kushinda moja.

Wakati huo huo Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinatarajiwa kuwasili leo saa 8 usiku kuamkia kesho katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. JK Nyerere kikitokea nchini Chad kilipokuwa na mchezo dhidi ya wenyeji jana jioni.

Msafara wa Taifa Stars unaongozwa na mkuu wa msafara ambaye pia ni Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina utaondoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa N’Djamena saa 8 mchana kuelekea Addis Ababa nchini Ethiopia, kabla ya kuunganisha ndege saa 4 usiku tayari kwa safari ya kurejea nyumbani Tanzania.

Stars inarejea nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya wenyeji Chad, bao lililofungwa na nahodha Mbwana Samatta katika mchezo uliochezwa uwanja wa Omnisport Idriss Mahaymat Ouya jijini N’Djamena katika mchezo wa kundi G kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017.

Mara baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, kikosi cha Taifa Stars kitaingia moja kwa kwa moja kambini katika hoteli ya Urban Rose iliyopo eneo la Kisutu kujiandaa na mchezo wa marudano utakaochezwa siku ya Jumatatu ya Pasaka katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.