Rais wa TFF Jamal Malinzi
Mkutano wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenyeviti wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kupata maoni yao juu ya changamoto zilizojitokeza katika ligi hiyo umefanyika juzi (Mei 11 mwaka huu).
Klabu za VPL zilizohudhuria mkutano huo ni Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Polisi Morogoro, Ndanda FC, Ruvu Shooting, Stand United na Tanzania Prisons.
Simba na Yanga hazikuhudhuria mkutano huo, na wala klabu hizo hazikutoa udhuru wowote wa kutokuwepo.
Maazimio ya mkutano huo ni kuwa kwa misimu mitatu ijayo kuanzia msimu wa 2014/2015 klabu zimekubaliana ziruhusiwe kusajili wachezaji watano wa kigeni. Kamati ya Utendaji ya TFF itatoa uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo katika kikao chake kijacho.
Pia klabu hizo zimekubali timu zao za U20 kuanzia msimu ujao zicheze ligi ya mkondo mmoja. Hata hivyo, utekelezaji wa hilo utategemea na upatikanaji wa mdhamini wa ligi hiyo ambapo TFF inafanya jitihada za kumpata mdhamini huyo.
Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake, Lina Kessy amezishauri klabu za VPL kuanzisha timu za wanawake, ambapo klabu hizo zimesema zitaufanyia kazi ushauri huo.
KIINGILIO MECHI YA TAIFA STARS 5,000/-
Kiingilio cha chini cha mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.
Washabiki watakaolipa kiingilio hicho ni kwa wale watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.
Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mechi hiyo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, na uwanja siku ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij inatarajia kurejea jijini Dar es Slaam kesho (Mei 14 mwaka huu) kutoka Mbeya kuendelea na maandalizi ya kuikabili Zimbabwe.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MKUFUNZI KASINDE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mkufunzi wa waamuzi nchini, Omari Kasinde kilichotokea jana (Mei 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mbali ya kuwa Mkufunzi, Kasinde ambaye anazikwa leo (Mei 13 mwaka huu) mchana katika Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyopita ya Waamuzi ya TFF iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Kapteni mstaafu Stanley Lugenge.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini kwani, Kasinde enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa katika mchezo huu tangu akiwa mwamuzi na baadaye mkufunzi na kiongozi..
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kasinde, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina.