Kikosi kamili cha timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania [Twiga Stars]
Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu “Twiga Stars” inatarajiwa kusafiri kesho Ijumaa kuelekea nchini Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wake wa marudiano wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Cameroon.
Kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars), leo kimefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Karume chini ya kocha mkuu, Nasra Juma tayari kwa safari ya kwenda kuwakabili timu ya Taifa ya Wanawake kutoka Zimbabwe (Mighty Warriors) katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika
Ikumbukwe Twiga Stars ilipoteza mchezo wa kwanza uliopigwa majuma mawili yaliyopita katika dimba la Azam complex Chamazi jijini Dar es Salaam baada ya kukubali kichapo cha bao 2-1 katika mchezo ambao Twiga stars iliweza kupata bao lake la kwanza mbele ya Wazimbabwe hao kwani mara zote Zimbabwe wamekuwa wakiifunga Twiga kwa mabao mengi nyumbani na ugenini huku Twiga ikitoka patupu.
Na hivyo sasa ili timu hiyo ivuke ni lazima Twiga Stars ipate ushindi katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumapili, Machi 20 katika uwanja wa Rufalo uliopo jijini Harare ili kuweza kufuzu kwa hatua ya pili ya michuano hiyo.