Saturday , 26th Dec , 2015

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anatarajia kusaini Mkataba wa miaka minne na nusu kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji iwapo Klabu yake ya sasa ya TP Mazembe na klabu hiyo zitaafikiana kuhusu pesa za kumuuza mchezaji huyo.

Wakala wa mchezaji huyo Jamal Kasongo amesema, Samatta ameshaafikiana na Klabu ya Genk na ameshasaini mkataba wa kwenda kuitumikia lakini mpaka sasa inasubiriwa makubaliano ya timu mbili ili Samatta aweze kuondoka Januari hapo mwakani.

Kasongo amesema, hapo awali klabu ya TP Mazembe walitaka walipwe ada ya uhamisho ya Euro milioni mbili na nusu ambapo Genk waliona ni nyingi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyobaki ambapo Genk waliweka dau la Euro laki tatu na nusu ambapo TP Mazembe imeona ni ndogo huku wakiwataka Genk waongeze dau ambapo Genk wataweka dau jingine siku ya Jumatatu.

Kasongo amesema, iwapo hawataafikiana itabidi Samatta asubiri aondoke majira ya joto akiwa mchezaji huru au aanze utaratibu wa kununua mkataba wake.

Samatta mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na Mazembe mwaka 2012 akitokea Simba SC ya jijini Dar es salaam, ambayo aliichezea kwa msimu mmoja pekee baada ya kujiunga nayo akitokea African Lyon, zamani Mbagala Market.