Friday , 6th Nov , 2015

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Jumapili kinatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya University of Pretoria (Tucks FC) jijini Johannesuburg ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Algeria.

Kikosi cha Stars kikiendelea na mazoezi Uwanja wa kituo cha michezo cha Edenvale Afrika Kusini

Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya progamu ya kocha mkuu, Charles Mkwasa baada ya kufanya mazoezi na vijana wake kwa takribani siku nne mpaka sasa ambapo anahitaji kuona maendeleo ya kikosi chake kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo dhidi ya Mbweha wa Jangwani Algeria.

Katika taarifa yake, Mkwasa amesema anashukuru maendeleo ni mazuri vijana wake wote wapo katika hali nzuri hakuna majeruhi na wanaendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya Algeria utakaopigwa Novemba 14 jijini Dar es salaam.

Mkwasa amesema, dhumuni la kuweka kambi Afrika Kusini ni kupata nafasi ya kuwaandaa vijana kwa mazoezi katika mazingira mazuri ikiwamo viwanja vya mazoezi, chakula na malazi kinachopelekea kuongezeka kwa umakini katika mazoezi.

Mkwasa amesema, wameanza na mazoezi ya kujenga utimamu wa mwili, nguvu na stamina kwa wachezaji, pumzi ili kuhakikisha vijana wote wanakuwa katika kiwango sawa (fitness level) kisha wataendelea na mazoezi ya kiufundi kwa siku zilizosalia kabla ya kurejea nyumbani.

Wachezaji 26 waliopo kambini ni magolikipa Ally Mustafa, Aishi Manula na Said Mohamed, walinzi ni Shomari Kapombe, Juma Abdul, Ramadhan Kessy, Mohamed Hussein, Mwinyi Haji, Hassan Isihaka, Salim Mbonde, Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub “Cannavaro”.

Wengine ni Himid Mao, Frank Domayo, Mudathir Yayha, Salum Abubakar, Said Ndemla, Jonas Mkude, Salum Telela, Farid Musa, Saimon Msuva, Malimi Busungu, Elias Maguri, John Bocco na Mrisho Ngasa.

Aidha wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea klabu ya TP Mazembe ya Congo DR, wanatarajiwa kuungana na kikosi cha Stars baada ya mchezo wao wa fainali Ligi ya Mabingwa Afrika Jumapili dhidi ya USM Algiers.