Friday , 27th Jun , 2014

Kocha mkuu wa Yanga Marcio maximo amesema hana tena tatizo na golikipa wa timu hiyo Juma Kaseja na kwamba tofauti zao za awali zimekwisha na sasa wanatazama mbele.

Kocha Marcio Maximo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwl Nyerere DSM

Klabu ya soka ya Yanga hii leo imemtambulisha rasmi kocha mkuu mpya wa klabu hiyo Mbrazil Marcio Maximo ambaye alitua nchini hapo jana tayari kuanza kazi ya kukinoa kikosi cha wanajanwani hao.

Wakala wa kocha huyo Barani Afrika Ally Mle amesema ujio wa Maximo ulikuwa ni mchakato wa muda mrefu na ulianza miaka mitatu iliyopita kwa kupitia changamoto nyingi lakini hatimaye sasa kocha huyo ametua nchini na kusaini mkataba wa miaka miwili.

Naye kocha Marcio Maximo amesema amekuja Yanga kuhakikisha anaipa mafanikio katika medani ya kitaifa na kimataifa kwani anatambua timu hiyo ni kongwe barani Afrika na ni moja ya timu yenye mipango ya muda mrefu ya maendeleo katika soka.

Aidha Maximo amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wawe wavumilivu katika kipindi hiki ambacho atakuwa anaijenga timu hiyo na wasitegemee miujiza.

Kwa upande mwingine kocha mkuu mpya wa klabu ya Yanga Mbrazil Marcio Maximo amesema hana tena tofauti na kipa mkongwe wa klabu hiyo Juma Kaseja kwani kilichotokea kimepita na sasa wanaganga yajao ili kuhakikisha Yanga inapata mafanikio.

Aidha Maximo amesema amefarijika sana kufanya kazi na makipa watatu wa klabu hiyo wenye uzoefu mkubwa na aliowahi kufanya nao kazi kwa nyakati tofauti katika timu ya taifa ya Tanzania, taifa stars na hivyo uwepo wa Kaseja ambaye ni kipa mkongwe na mzoefu kutasaidia kumjenga zaidi kipa namba moja wa timu hiyo kwa sasa Deogratius Munishi ‘Dida’