Saturday , 19th Mar , 2016

Hatimaye timu ya soka ya Simba imefanikiwa kuzoa pointi zote 18 baada ya kufanikiwa hii leo kuifunga tena timu ya Coastal Union na kuweka rekodi kwa mara ya kwanza msimu huu kuzichapa timu zote tatu za Tanga nyumbani na ugenini.

Mshambuliaji anayeongoza kwa ufungaji katika ligi kuu bara kwa sasa Hamis Kiiza wa Simba SC.

Kipigo cha bao 2-0 walichoipa timu ya wagosi wa kaya Coastal Union ya Tanga katika mchezo uliopigwa katika dimba la Mkwakwani timu ya Simba imejiwekea rekodi yake binafsi kwa mara ya kwanza kufanikiwa kuzifunga timu zote za Tanga katika michezo ya nyumbani na ugenini.

Simba ambayo ilikuwa haijawahi kushinda kwa muda mrefu misimu kadhaa ikicheza na timu za Tanga katika dimba la Mkwakwani ilianza kufuta hali hiyo mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuifunga African Sports kwa bao 1-0 na baadaye ikaifunga timu hiyo bao 4-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa jijini Dar es salaam.

Rekodi ya Simba iliendelea katika mchezo wake dhidi ya maafande wa JKT Mgambo walipowafunga mabao 2-0 katika uwanja huo huo wa Mkwakwani na kushinda tena kwa jumla la mabao 5-1 katika mchezo wa marudiano uliopigwa katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam.

Magoli ya mshambuliaji wa zamani wa Coastal Unioni ambaye hii leo alirejea nyumbani Danny Lyanga kunako dakika 39 na lile la dakika 52 kipindi cha pili la kinara wa upachikaji mabao katika ligi kuu Mganda Hamis Kiiza ambaye sasa ametimiza magoli 19 yalitosha kuiwezesha Simba kufikia rekodi yake ya kwanza kwa kushinda michezo yote dhidi ya timu za Tanga katika uwanja wa Mkwakwani na pia kuzifunga nyumbani na ugenini na kutwaa alama zote 18.

Kocha mkuu wa Simba Mganda Jackson Mayanja ambaye aliwahi kuinoa timu ya Coastal Union katika mchezo huo wa leo alifanya mabadiliko kidogo katika kikosi chake huku akimwanzisha Danny Lyanga kuchukua nafasi ya mshambuliaji hatari wa timu hiyo Ibrahim Ajib Migomba ambaye alikuwa benchi, lakini pia beki wake kisiki wa upande wa kulia Hassan Ramadhan Kessy ambaye nafasi yake ilishikwa na Mrundi Emiry Nimubona.

Kwa ushindi huo sasa Simba SC imeendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa pointi saba zaidi ya wapinzani wao Azam na Yanga katika mbio za ubingwa.

Msimamo wa ligi hiyo kwa timu tatu za juu unaonyesha kuwa mpaka sasa Simba SC imefikisha pointi 57, baada ya kucheza mechi 24, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 50 sawa na Azam FC baada ya timu zote hizo kucheza mechi 21 zikitofautiana kwa idadi ya magoli yakufunga na kufungwa.

Na kwa kipigo hicho cha leo Coastal Union iliyozifunga timu za Yanga kwa mabao 2-0 na Azam kwa bao 1-0 katika uwanja wa Mkwakwani, sasa timu hiyo maarufu kama wagosi wa kaya ambao awali walichapwa na Simba bao 1-0 katika uwanja wa taifa sasa wanabakia na pointi zao 19 ambazo ni sawa na idadi ya mabao ya mfungaji anayeongoza kwa sasa Hamis Kiiza baada ya kucheza mechi 24 na hivyo kuendelea kuburuza mkia katika Ligi Kuu Tanzania bara yenye timu 16.

Matokeo ya mechi nyingine zilizopigwa leo ni kama ifuatavyo:-

Stand United 1 - 1 Ndanda FC
Majimaji FC 3 - 1 Mbeya City