Wednesday , 6th Apr , 2016

Katika suala ambalo limekuwa kero kwa baadhi ya vilabu vya ligi kuu ya soka Tanzania bara ni suala la mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba na moja ya timu iliyolalamikia hali hiyo ni vinara wa ligi hiyo timu ya soka ya Simba wakisema kuna hujuma.

Mkuu wa Idara ya habari wa Simba sc Haji Manara akimkabidhi barua ya malalamiko ya ratiba ya ligi kuu Waziri Nape Nauye.

Klabu ya soka ya Simba imesema kuanzia sasa haitatuma barua bodi ya ligi wala TFF kuomba marekebisho ya ratiba ya ligi kuu na hivyo wameamua kwa kauli moja kuendelea kucheza kwakuwa kufanya hivyo hakutawasaidia kwani tayari kuna mazingira ya wazi kwa bingwa kupangwa.

Akiongea kwa kujiamini mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo Haji Manara amesema hivi sasa mpira umeingiliwa hasa hapa nchini ukiangalia mambo yanapelekwa bila kuzingatia weledi wa soka hasa katika suala la upanguaji wa mara kwa mara wa ratiba tena usio na sababu za kimsingi.

Amesema "Eti timu flani inaomba kusogezewa mchezo wake mbele kisa ina mchezo mgumu wa kimataifa ikitaka ijiandae na kuongeza idadi ya michezo ya viporo kwa baadhi ya timu".

Manara amesema tangu kuanza kwa ligi kuu Tanzania bara msimu huu mnamo mwezi Septemba ligi ambayo awali kabla ya mabadiliko ya ratiba ilikuwa ianze mwezi Agost basi tangu wakati huo imekuwa ndiyo ligi pekee ambayo ina rekodi ya ratiba yake kubadilishwa mara kwa mara haijawahi kutokea duniani kote ratiba ya ligi kubwa kama VPL kufanyiwa mabadiliko kama ya ligi yetu hivi sasa.

Aidha Manara amesema inashangaza kuona klabu fulani inatuma barua bodi ya ligi na TFF kuomba iende kwenye ziara ya michezo ya kirafiki ama nyingine ikiomba ikaweke kambi ya kujiandaa na mchezo wa kimataifa na kusababisha timu hizo kuwa na michezo mkononi maarufu kama viporo kitu ambacho si sahihi kwa mustakabali wa soka kwa kuwa timu nyingine zitakuwa zikiendelea na ligi kwa ushindani huku zilizo na viporo ikifika wakati wa kucheza michezo yao hiyo pengine kukawa hakuna ushindani.

Manara akaenda mbali zaidi akisema ukiachilia mbali suala la Azam kwenda DR. Congo kwenye michezo ya kirafiki wakati ligi ikiendelea lakini suala la juzi bodi ya ligi na TFF kuikubalia klabu ya Yanga iliyoomba mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar uliokuwa upigwe jijini Dar es Salaam jumatano April 06 na kuusogezwa mbele hadi April 16 ni suala linalotia shaka hasa ikizingatiwa kuwa Yanga hao ambao wameomba kucheza April 16 na Mtibwa siku tatu baadae watakuwa na kibarua ugenini kucheza mchezo wa marudiano wa kuwania klabu bingwa barani Afrika dhidi Al Ahly utakaopigwa jijini Cairo April 19.

Manara amesema "Kwa hali hiyo ni wazi kuwa suala la kubadilisha ratiba liko pale pale kwani ukiangalia muda wa mchezo huo na Yanga wasafiri kwenda Cairo ni kitu ambacho haiingii akilini mwa mtu yeyote timamu hivyo ni wazi mchezo huo ni lazima utaahirishwa na ni mpango dhahili wa bodi ya ligi na TFF kuhakikisha Yanga inatetea ubingwa wa ligi hiyo kitu ambacho si sahihi kimpira" aling'aka Manara ambaye ni mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa timu ya Yanga na taifa Stars Sunday Manara Computer.

Kwa upande mwingine Manara amesema kufuatia kipa wao chipukizi Denis Richard aliye kwa mkopo katika klabu ya Geita iliyoshiriki ligi daraja la kwanza FDL kufungiwa na kamati ya nidhamu ya TFF kwa miaka kumi kujihusisha na mchezo wa soka kutokana na kukutwa na hatia ya kuhusika na upangaji wa matokeo ya mchezo wa mwisho wa kundi C baina ya timu yake na JKT Kanembwa na wao kama Simba wanasema ni lazima taasisi ya kupambana na rushwa TAKUKURU watue TFF kufanya uchunguzi zaidi kwani kuna taarifa za wahusika wengine ambao hawajajumuishwa katika zoezi hilo na wengi wao wakiwa ni viongozi wa juu na maofisa wa TFF.

Akimalizia Manara amesema hawako katika kumtetea kipa wao kwamba ameonewa lakini ni vema kutokana na clip za sauti na taarifa zilizozagaa kwa sasa katika mitandao ya kijamii zikiwataja moja kwa moja na wazi wazi viongozi na maofisa wa TFF kuhusika na kadhia hiyo basi zifanyiwe kazi haraka na TAKUKURU na hata kama kipa wao huyo ama mtu yeyote akipataikana na hatia hiyo basi apewe adhabu kali si tu kufungiwa maisha bali afutwe kabisa katika medani ya soka.