Wanamichezo wa michezo ya sanaa za mapigano wakionyesha umahili wao.
Chama cha mchezo wa Wushu Tanzania TWA kimesema pamoja na kuahirisha shindano la kimataifa la mabingwa wa mabingwa yaliyokuwa yafanyike mwishoni mwa mwezi ujao sasa watafanya shindano maalumu la kufunga mwaka litakaloshirikisha wachezaji wa ndani pekee.
Katibu mkuu wa TWA Sempai Gola Kapipi amesema shindano hilo ambalo litashirikisha mabingwa wa michezo ya sanaa zote za mapigano kwa wachezaji wa ndani, halitahusisha wachezaji toka nje ya nchi kama ilivyokuwa lile ambalo limeahirishwa.
Miongoni mwa michezo ya sanaa za mapigano itakayohusika katika tamasha hilo maarufu kama bingwa wa mabingwa ni pamoja na michezo ya judo, karate, ngumi, ngumi na mateke na wushu yenyewe ambayo inajumuisha aina zote za michezo ya kung fuu na shaoling.
Aidha Kapipi amesema lengo kubwa la shindano hilo si tu kuwashindanisha mabingwa wa michezo hiyo bali pia kukutana na kuunda umoja na kushirikiana katika kupeana uzoefu wa aina na mitindo tofauti ya sanaa zao huku pia wakiwa na lengo la kutengeneza lengo moja la kuweka nguvu katika kushawishi wadau na serikali kuweza kuwaunga mkono wanamichezo wa michezo mingine kama yao na kuiwezesha kufanya vema zaidi kitaifa na kimataifa.
Akimalizia Kapipi amesema ujumbe wao mkubwa ni kuwakumbusha wadau kudhamini michezo ya sanaa za mapigano kwakuwa ndiyo michezo pekee ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika medani ya kimataifa tofauti na michezo mingine inayotazamwa sana akitolewa mfano , mpira wa miguu ambao amesema umekuwa ukipata udhamini kila kukicha lakini matokeo yake Tanzania inaishia kuwa wasindikizaji.