Wednesday , 8th Apr , 2015

Timu ya Ruvu Shooting imesema imeshajipanga kwa ajili ya kuchukua Pointi tatu muhimu katika mechi zilizobakia za ligi kuu soka Tanzania Bara inayoelekea ukingoni.

Katika taarifa yake, Afisa habari wa Timu hiyo, Masau Bwire amesema, kikosi kinajiandaa na mechi dhidi ya Kagera itakayochezwa Jumamosi wiki hii uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ambapo kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo itakayokuwa na ushindani mkubwa.

Bwire amesema Kagera ni moja ya timu ngumu inayocheza kitimu na yenye wachezaji wanaojiamini na wenye uchu wa kufumani nyavu lakini kikosi chake kimejidhatiti kwa kila idara kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo.

Bwire amewataka waamuzi wa mchezo huo kuchezesha kwa kuzingatia sheria 17 za soka ili kila timu ipate inachostahili kutokana na uwezo.

Kikosi cha Ruvu Shooting kinatarajia kuelekea kesho Mjini Shinyanga kikiwa na jumla ya wachezaji 20 na viongozi 10 huku wachezaji saba wakiachwa kutokana na sababu mbalimbali.

Wachezaji ambao hawataungana na kikosi hicho hapo kesho ni Golikipa namba moja Abdallah Rashid Babu na Salvatory Mtebe ambao wanakadi tatu za njano, Juma Mpakala ambaye yupo katika matatizo ya kifamilia, Betram Mombeki, Stephano Mwasyika, Lambele Jarome na Juma Abdul ambao ni majeruhi.