Timu kubwa kutoka ligi nne kubwa barani Ulaya
Hivi sasa ligi mbalimbali zikielekea ukingoni, kila timu inajitahidi kupambana itimize lengo lake, zipo zile ambazo kwa lugha ya mtaani tunasema 'ZIPO CONSTANT' kila msimu kazi yao ni kupigania zisishuke daraje, zipo zinazopambana kumaliza nafasi nne za juu ili kupata nafasi ya kucheza Klabu Bingwa Ulaya lakini pia zipo zile zinazopigania kubeba taji la ligi husika.
Tukianza na ligi pendwa duniani, ligi kuu ya Uingereza EPL, Jumapili hii kutakuwa na vita kali yenye faida katika pande mbili, upande wa mbio za ubingwa na upande wa mbio za kumaliza 'TOP FOUR', pale ambapo Manchester City inayopumulia sikioni mwa Liverpool itakapovaana na Chelsea ambayo inajitahidi kupona taratibu kutokana na kuweweseka na Alvaro Morata, ambaye mashabiki wake wanaamini amewanyima mabao mengi msimu huu.
Mpaka sasa Man City inaongoza ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Liverpool iliyo nafasi ya pili, ikikaa kileleni kwa mara ya kwanza tangu Desemba 15 mwaka uliopita. Chelsea nayo iko chumba mahututi katika nafasi ya nne, kwani endapo itatoka sare au kupoteza mchezo huo, ugali wao unaweza kutiwa mchanga na Man United iliyo nyuma kwa pointi mbili katika nafasi ya tano.
Kesho Jumamosi, Man United itaingia 'TOP FOUR' kwa mara ya kwanza msimu huu endapo itapata ushindi dhidi ya Fulham huku Liverpool iliyo katika 'Pressure' kubwa ya ubingwa hivi sasa, ikizisaka alama tatu dhidi ya AFC Bournemouth katika dimba la Anfield ili kurejea kileleni. ina rekodi nzuri katika uwanja wake wa nyumbani msimu huu, ikicheza mechi 12 mpaka sasa za ligi ikiwa haijapoteza mechi yoyote.
Arsenal ambayo imekaribishwa mtaa wa sita na Man United, itavaana na Huddersfield Town inayoburuza mkia na iliyo na rekodi mbovu ya kupoteza mechi nne kati ya tano za mwisho za ligi.
Southampton inayoendelea kuimarika siku hadi siku itapambana na Cardiff City ambayo leo kwa mujibu wa ripoti za polisi, imempoteza rasmi mchezaji wake, Emiliano Sala baada ya uchunguzi wa mabaji ya mwili kuonesha ni ya mchezaji huyo.
Michezo mingine hapo kesho ni: Crystal Palace dhidi ya West Ham United, Watford na Everton pamoja na Brighton dhidi ya Burnley.
Katika La Liga wikiendi hii, masikio na macho ya wengi ni katika 'DERBY' ya watoto wa mji mmoja, Atletico Madrid na Real Madrid utakaopigwa katika dimba la Wanda Metropolitano. Timu hizi zimepisha alama 2 pekee, hali ambayo inaufanya mchezo huo kuwa wa kuvutia, atakayeshinda atamkaribi Barcelona alie kileleni kwa pointi 50, ambaye atashuka dimbani Jumapili dhidi ya Athletic Club Bilbao.
Michezo mingine ya Laliga Jumamosi hii ni: Getafe dhidi ya Celta Vigo, Espanyol ikiwakaribisha Rayo Vallecano na Girona dhidi ya Huesca.
Katika Bundesliga wikiendi hii, vinara Borussia Dortmund itapambana na TSG Hoffenheim, huku Freiburg ikiwakaribisha Wolfsburg, Hannover 96 dhidi ya Numberg, RB Leipzig ikipambana na Entracht Frankfurt, Borussia Monchengladbach dhidi ya Hertha Berlin na mchezo wa mwisho, kigogo Bayern Munich ambaye haonekani kufanya vizuri msimu huu atapambana Schalke 04.
Katika Serie A, wikiendi hii Kinara wa ligi, Juventus atasafiri ugenini kucheza dhidi ya Ssasuolo ambapo ikishinda mchezo huo itafikisha pointi 63, AC Milan dhidi ya Cagliali, Torino dhidi ya Udinese, Sampdoria dhidi ya Frosinone, Atalanta dhidi ya Spal, Bologna na Genoa na mchezo mkali wa mapema zaidi Jumamosi ni kati ya Fiorentina watakapoikaribisha Napoli ya Carlo Ancelloti huku Parma ikiwakaribisha Inter Milan.






