Monday , 26th Jan , 2015

MICHUANO ya mpira wa Miguu kwa wanawake ya Taifa Cup inaingia leo katika hatua ya Robo Fainali kwa kushirikisha timu kutoka mikoa nane hapa nchini.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya soka la wanawake Tanzania, Blasi Kiondo amesema timu zote zilizoingia katika hatua hiyo ya Robo Fainali zimeshawasili jijini Dar es salaam ambapo mechi zote zitapigwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam.

Kiondo amesema, katika michuano hiyo kila timu itacheza dakika 40 kipindi cha kwanza na dakika 40 kwa kipindi cha pili ambapo itakuwa ni dakika 80 kwa mechi ambapo kama timu zikitoka sare zitaingia katika hatua ya matuta na timu itakayofungwa itakuwa imeaga mashindano hayo.

Kiondo amesema michuano hiyo inalenga kukuza na kutafuta vipaji vipya vya timu za wanawake hapa nchini.

Kiondo amesema, michuano hiyo ya hatua ya Robo Fainali itachezwa kwa siku mbili ambapo kila siku zitachezwa mechi mbili ambapo mchezo wa kwanza unaoanza leo mchana utakutanisha timu ya Mwanza ikipambana na Kigoma huku mchezo utakaofuata ambao utachezwa jioni utawakutanisha Tanga na Pwani na huku kesho ikizikutanisha Ilala na Iringa na katika mechi ya jioni ikizikutanisha Mbeya na Temeke.

Kwa upande wake Kocha wa Timu ya Iringa Queens, Fidelis Kalinga amesema, kila timu imejipanga kwa ajili ya kupambana ili kuweza kuibuka na ushindi hivyo anaamini wataweza kuibuka na ushindi dhidi ya Ilala na hatimaye kuingia hatua ya Nusu Fainali na kupita hadi fainali na kuchukua Kombe.