Mshambuliaji hatari wa timu ya Simba Mganda Emmanuel Okwi akimpiga chenga beki wa Gor Mahia ya Kenya.
Hali hiyo ilionekana kumpa taabu kidogo Okwi katika dakika za mwanzo wa mchezo huo na kushindwa kucheza vizuri na kuonesha cheche zake, lakini baadaye aliweza kutulia na kuanza vitu vyake na kujikuta anakuwa chachu ya ushindi wa Simba SC katika mchezo huo mkali kabisa uliopigwa katika uwanja wa taifa jioni ya leo
Katika mchezo huo vinara hao wa ligi kuu ya Kenya Gor Mahia walianza vizuri wakitawala mchezo hususani katika safu ya kiungo, lakini safu imara ya ulinzi ya Simba SC chini ya Nahodha Joseph Owino na kinda Rajabu Isihaka ilikuwa kikwazo kwao kupata mabao huku sifa zaidi zikimwendea kipa Ivo Mapunda aliyeokoa michomo mingi ya hatari iliyokuwa ikielekezwa langoni mwa Simba na washambuliaji hatari wenye uchu wa Gor Mahia wakiongozwa na Mganda Dan Sserunkuma
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Patrick Phiri kunako dakika ya 34 kwa kumtoa kiungo mkabaji kinda William Lucian ‘Gallas’ na kumuingiza winga teleza Uhuru Suleiman aliyekwenda kucheza pembeni kwa Awadh Juma aliyeingia kati , yaliibadilisha kabisa Simba SC kwa ujumla na kuanza kutakata kiwanjani na hivyo kuibua shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo
Mganda Okwi ambaye hatima yake ya kuchezea Simba katika ligi kuu Tanzania bara itajulikana kuanzia Septemba 7 mwaka huu akaingia ndani na Uhuru akawa anashambulia akitokea pembeni kushoto, huku Ramadhan Singano Messi akikimbiza kupitia winga ya kulia-na hapo Simba SC ikawa moto kwa Gor Mahia kwa muda wote hasa kipindi cha pili
Ambapo katika kipindi cha pili kocha mzambia Patrick Phiri alianza na mabadiliko ambapo kipindi hicho alimpumzisha mshambuliaji Elias Maguri na nafasi yake kuchukuliwa na Mkenya, Paul Kiongera, aliyekuwa shujaa wa mchezo
Kiongera alifunga bao la kwanza dakika ya 52 akiunganisha krosi ya Okwi aliyemlamba chenga na kumtoroka vizuri beki wa Gor pembeni kushoto
Messi akafunga la pili dakika ya 67 akiuwahi mpira uliotemwa na kipa Frederic Onyango kufuatia shuti la Okwi aliyemalizia krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kabla ya Kiongera kumalizia vizuri krosi ya Uhuru dakika ya 78 kuipatia Simba SC bao la tatu
Kwa Kiongera huu unakuwa mchezo wa pili tangu ajiunge na Simba SC baada ya awali kucheza katika Simba Day, Wekundu wa Msimbazi walipocheza na Zesco United ya Zambia
Kwa kocha Phiri, huu unakuwa mchezo wa Nne tangu arejee Simba SC mwezi uliopita na ameshinda mechi zote, awali alishinda bao 2-1 dhidi ya Kilimani FC,na baadae wakashinda bao 2-0 dhidi Mafunzo na wakaishindilia bao 5-0 timu ya KMKM zote za Zanzibar.