Saturday , 29th Aug , 2015

Kiungo chipukizi wa Yanga SC, Said Juma Makapu amesema hivi sasa anajiona yuko fiti kabisa kucheza soka la ushindani na kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa.

Katika taarifa yake Makapu amesema, hali aliyokuwa nayo tangu alipoumia mgongo katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara msimu uliopita dhidi ya Ndanda FC Mjini Mtwara na sasa anaona inazidi kuimarika hivyo anaamini msimu ujao atakuwa amepona kabisa na kurejea akiwa na afya uwanjani.

Makapu alishindwa kuichezea timu ya taifa katika michuano ya Kombe la COSAFA nchini Afrika Kusini katikati ya mwaka huu na akakosa michuano ya Kombe la Kagame timu yake ikitolewa Robo Fainali.

Makapu alirejea uwanjani baada ya Kombe la Kagame na kucheza mechi zote za kirafiki mjini Mbeya, Yanga ikishinda 4-1 dhidi ya Kemondo, 3-2 dhidi ya Mbeya City na 2-0 dhidi ya Prisons huku mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC wiki iliyopita akiingia na akaiongoza Yanga SC kushinda kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.