Wednesday , 23rd Jul , 2014

Nilitaka kupumzika baada ya pambano langu na bondia wa Thailand, lakini isingekuwa vyema kupumzika baada ya kupigwa. Hivyo baada ya kushinda pambano langu na Mohamed Matumla, nikaona ngoja npumzike, hata meneja wangu alinishauri hivyo"

Francis Miyeyusho akiwa hoi baada ya kupigwa kwa TKO na Sukkassem Kietyongyuth wa Thailand. Hii ilikuwa April 19 mwaka huu katika ukumbi wa PTA-Sabasaba. Pambano hilo halikuwa la ubingwa.

Bondia wa uzito wa "Feather" ambaye kwa sasa amepanda mpaka uzito wa "Batam", Francis Miyeyusho, amesema kwa sasa anavuta pumzi ili akirejea ulingoni arudi kwa kishindo kizito.

Miyeysho ambaye mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa May 10 mwaka huu dhidi ya Mohamed Matumla pambano ambalo alishinda kwa pointi, amesema anataka mashabiki wake 'wammis' ili wawe na hamu naye.

Aidha bondia huyo maarufu kama Chichi Mawe, ameomba promota atakayejitokeza kumuandalia pambano, amuandalie pambano dhidi ya bondia wa nje kwani mabondia wa hapa nyumbani wa uzito wake ameshawapiga wote.

"Nataka niwanie ubingwa wa dunia kama anavyofanya Francis Cheka, hapa nyumbani hakuna bondia mwenye uwezo wa kupigana na mimi". Amesema Miyeyusho

Alipoulizwa maoni yake kuhusu kesi inayomkabili Francis Cheka kutokana na kufanya shambulio la kudhuru mwili huko Morogoro, Miyeyushoa amesema hajapata nafasi ya kuongea na Cheka kujua nini hasa kilikuwa chanzo cha ugomvi huo, lakini anaomba asamehewe kwani kesi hiyo inamfanya apoteze muda mwingi kuifuatilia hivyo kukosa mapambano.

Miyeyusho amecheza mapambano 51 tokea aanze kupigana masumbwi ya kulipwa Februari 1, mwaka 1998. Ameshinda mapambano 37, kati ya hayo 23 kwa KO na kupigwa 11, kati ya hayo 10 kwa KO na ametoka sare mara mbili.