Friday , 26th Dec , 2014

Mikoa 13 imethibitisha kushiriki mashindano ya Taifa ya Netball ambayo yanatarajiwa kuanza Januari mwakani Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Mwenyekiti wa Chama cha Netball Nchini CHANETA, Anna Kibira amesema awali ilikuwa mikoa mitano pekee ambayo ilikuwa imethibitisha kushiriki mashindano hayo ila hadi kufikia jana jumla ya mikoa 13 imethibitisha ushiriki wake.

Kibira aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Kinondoni, Ilala, Temeke, Katavi, Dodoma, Arusha, Lindi, Mwanza, Mara, Tabora, Pwani, Kusini Unguja na Mjini Magharibi.

Kibira amesema bado anaomba wadau mbalimbali wajitokeze kuisaidia CHANETA mahitaji mbalimbali ambayo yatasaidia ufanikishaji wa mashindano hayo.

Kibira amesema pamoja na wadau, pia wanaiomba Serikali kuhakikisha kwamba mashindano hayo yatasaidia kupatikana kwa timu ya Taifa ya Mchezo wa Netball nchini.