Sunday , 3rd May , 2015

Bondia mmarekani Floyd Mayweather leo ametwaa taji la Ubingwa wa ndondi la Walter weight, linalotambuliwa na Shirikisho la Masumbwi Duniani – WBC baada ya kumshinda kwa alama nyingi, hasimu wake wa muda mrefu, bondia mfilipino Manny Pacquiao.

Mayweather akinyoosha juu mkono kama ishara ya ushindi muda mfupi baada ya pambano hilo kufikia mwisho.

Wengi walidhani kuwa Pacquiao anayetambulika kwa upigaji wa ngumi za harakaharaka pengine angeibuka bingwa wa pambano hilo la raundi kumi na mbili lakini hali ikawa tofauti kwa mmarekani huyo ambaye tangu mizunguko ya awali alionnesha dalili za kutaka kushinda.

Pambano hilo lililofanyika majira ya alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki limevuta watazamani wengi na linatajwa kuwa ni pambano la kihistoria kwa kukusanya kiwango kikubwa cha mapato na likiwa na thamani ya Pauni milioni 300 za Uingereza, zaidi ya fedha za Tanzania shilingi bilioni 600.

Akizungumza baada ya kutwaa taji la ubingwa, Mayweather amesema atacheza pambano moja baadaye Septemba mwaka huu, pengine likiwa ndilo pambano lake la mwisho kabla ya kustaafu masumbwi.

Wachambuzi wa masuala ya mchezo wa masumbwi wanasema baada ya kukosa ubingwa huo, faraja pekee aliyobakia nayo Pacquiao ni mapato atakayolipwa baada ya pambano hilo ambapo kwa mujibu wa waandaaji, jumla ya dola milioni 230, zaidi ya fedha za Tanzania shilingi bilioni 400 zimetengwa kwa ajili ya mabondia hao wawili.