Friday , 13th May , 2016

Ufundi mwingi wa kuchezea mpira na ujuzi unaochangiwa na bidii na kujiamini kwa mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajib kumeanza kuwapagawisha viongozi wa benchi la ufundi na wachezaji wa timu ya Golden Arrows FC ambao wameonekana kuvutiwa haraka na Ajib.

Mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajib akiwa katika uwanja wa mazoezi wa timu ya Golden Arrows ya Afrika Kusini.

Kocha wa timu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini ABSA , Clinton Paul Larsen amevutiwa na uchezaji wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Ajib, lakini amesema anahitaji kumuona zaidi.

Kocha huyo mzaliwa wa Durban, KwaZulu-Natal mwenye umri wa miaka 45, leo amekutana na Meneja wa mchezaji huyo wa Simba ya Tanzania na kumpa taarifa za awali kuwa Ajib anaonekana ni mchezaji mzuri, amevutiwa naye, ila anahitaji kuendelea kumuona zaidi kabla hajatoa majibu,”amesema Meneja wa Ajib, Juma Ndambile.

Ndambile amesema Ajib alifanya vizuri katika mazoezi yake ya kwanza na timu hiyo jana na leo pia ameendelea tena kuonyesha uwezo wa hali ya juu.

Akizungumzia mazoezi ya awali ya hapo Ndambile amesema “Jana hadi wachezaji wa ile timu walimfuata na kuanza kumpa moyo, wanamuambia anaweza na ni mchezaji mzuri unaweza kusajiliwa hapa [Afrika Kusini].

Ajib yupo nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kusaka timu ya kuchezea, mipango inayosimamiwa na wakala maarufu nchini humo, Rodgers.

Ajib ambaye ametua nchini humo bila baraka za viongozi wa timu yake ambayo bado anamkataba nayo wa mwaka mmoja itabidi awaangukie wanamsimbazi ili kupata baraka za kukipiga nchini humo.

Rodgers amewaalika Watanzania wawili kwa majaribio nchini humo, pamoja na Ajib mwingine ni kiungo chipukizi wa Azam FC, Omar Wayne ambaye tayari amefuzu majaribio katika klabu nyingine ya Ligi Kuu nchini humo, AmaZulu.

Hata hivyo, Wayne ameambiwa kutokana na umri wake mdogo inabidi asajiliwe kama mchezaji wa kikosi cha pili.

Wayne mwenyewe amesema anaweza kukubali kusajiliwa AmaZulu B, lakini wasiwasi wake ni kama klabu yake, Azam FC itakubali kumtoa bure.

Mustakabali wa Wayne unatarajiwa kujulikana leo baada ya kikao cha viongozi wa AmaZulu.