Bondia Thomas Mashali akiwa na moja ya mikanda aliyotwaa.
Bondia Thomas Mashali ambaye hivi karibu ameitwa katika timu ya taifa ya ngumi itakayoshiriki michuano ya kufuzu kwa Olimpiki ya Rio Brazil mwezi Agasti mwaka huu ametoa wito kwa mabondia wengine wa ngumi za kulipwa kujitokeza kwenda kulitetea Taifa katika michuano hiyo.
Mashali ambaye ni bingwa wa dunia wa mkanda wa UBO amesema alipopewa taarifa za kuitwa katika timu ya taifa kwaajili ya michuano ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Olimpiki ya Rio Brazil alikubali bila kusita kwakuwa alitambua wazi kuwa hiyo ndiyo itakuwa ni fursa kwake kujitangaza zaidi na kutangaza pia nchi kimataifa.
Mashali amesema mashindano ya Olimpiki ni mashindano yanayohusisha ulimwengu mzima hivyo ni fursa kwa mabondia wa ngumi za kulipwa[ maproo] kutumia michuano hiyo kujitangaza wao binafsi na taifa kwa ujumla.
Aidha Mashali amekiri kuwa michuano hiyo ya kufuzu ambayo itafanyika nchini Venezuela mapema mwezi ujao itakuwa migumu mno kwani ndiyo michuano pekee ya mwisho kwa wanamasumbwi kusaka tiketi ya kufuzu kwa Olimpiki ya Rio itakayofanyika mapema mwezi Agasti mwaka huu nchini Brazil, hivyo ni wazi kila mpiganaji atataka kupata nafasi hiyo adimu ya kuwakilisha nchini yake.
Akiendelea kuzungumza bondia huyo ambaye amesokota nywele zake kwa mtindo wa rasta amewataka mabondia watakaojitokeza kujiunga na timu ya taifa wajipange vyema kwajili ya kwenda kushindana na si kushiriki peke yake ili kuweza kutwaa nafasi hiyo adimu.
Ushiriki wa Mashali katika michuano hiyo ni kutokana na mabadiliko ya kanuni ya mchezo wa ngumi yaliyofikiwa baina ya vyama shiriki vya ngumi duniani na shirikisho la kimataifa la mchezo huo AIBA kuingiza ngumi za kulipwa ama kushirikisha ngumi za kulipwa na ridhaa ambapo sasa kwa mabadiliko hayo mchezaji wa ngumi za kulipwa anaweza kucheza ngumi za ridhaa na baadae kurejea katika ngumi za kulipwa.