
Mfaume Mfaume (kulia) katika moja ya pambano na Habibu Pengo (kulia)
Mfaume anayeshikilia mkanda wa Afrika Mashariki katika mizani ya uzito wa Welterweight alipoteza katika pambano dhidi ya Vaghinak Tamrazyan, lililopigwa Oktoba 27, nchini Urusi.
Akizungumza na www.eatv.tv iliyotaka kufahamu juu ya sababu ya kupoteza pambano hilo na kusuasua kwa mchezo wa ngumi nchini na bara la Afrika, Mfaume amesema.
"Nafikiri kwamba sio tatizo letu mabondia wa sasa au wa kipindi cha nyuma hapana, ila kuna kupoteza kwa aina nyingi pia, kama mnavyojua mabondia wa kiafrika wakitoka kwenda kupambana na mabondia wa nchi za Ulaya kunakuwa na hujuma, hata katika pambano langu mkiliona video, mtaona kabisa ni hujuma", amesema.
"Pia suala la kwenda nje bila ya kuwa na kocha ni sababu nyingine kwasababu ukienda na kocha anakuwa anakujua tofauti na kwenda na mtu mwingine tuu kunakuwa na upungufu", ameongeza.
Pia, Mfaume amewashauri mabondia mbalimbali wa Tanzania na bara la Afrika watakaoshiriki michuano ya ngumi ya dunia kutokubali kupangiwa waamuzi wanaotoka nchi moja na wapinzani wao kwakuwa, akidai kuwa hiyo ndiyo sababu inayopelekea kuhujumiwa.
Mfaume Mfaume anayeshikilia nafasi ya kwanza katika viwango vya ubora wa ngumi nchini kwa mambondia wa uzito wake, amepigana jumla ya mapambano 20 mpaka sasa, akishinda 13, akipoteza mapambano manne na mapambano mengine matatu yakimalizika kwa sare.