
Shaaban Idd Chilunda mchezaji wa Azam FC ambaye amesajiliwa Tenerife ya Hispania.
Akiongea na eatv.tv Shaaban Idd ambaye jana alifunga mabao 4 kwenye ushindi wa 4-2, iliopata Azam FC kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Kagame, ameweka wazi kuwa tangu apone majeraha yake amekuwa akijituma zaidi ili kuboresha kiwango chake.
''Nilipopata majeraha ya goti nilikuwa na uoga sana, kuwa nikipona nitapata nafasi kweli, ila nilipopona nikaamua kujituma zaidi ili nipate nafasi, baada ya hapo nikaaminiwa na kocha nikawa nafunga na kwasababu kila kocha anapenda mshambuliaji anayefunga basi nikawa nachezeshwa kila mechi'', - amesema.
Shaban Idd aliumia goti na kukosa raundi yote ya kwanza kwenye ligi kuu soka Tanzania bara wakati akipatiwa matibabu ya goti nchini Afrika Kusini na baada ya kurejea dimbani raundi ya pili alifanikiwa kufunga mabao 8 ikiwemo Hat-trick dhidi ya Tanzania Prison.
Muda wowote baada ya michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea, ambapo klabu yake imetinga hatua ya nusu fainali na kesho itacheza na Gor Mahia ya Kenya, Shaaban anarajia kuondoka nchini kwenda Hispania kuitumikia klabu ya Tenerife inayocheza Ligi daraja la kwanza ambayo tayari imeshamsainisha mkataba wa miaka miwili.