Friday , 1st May , 2015

Chama cha Mpira wa wavu Mkoa wa Dar es salaam, kimesema mpango wa kutoa kozi ya waamuzi wa mchezo huo wanatarajia kuendelea nao ili kuweza kupata waamuzi wengi watakaoweza kusimamia ligi mbalimbali zilizo katika ratiba ya mwaka.

Akizungumza na East Africa Radio, katibu wa DAREVA Yusuph Mkarambati amesema, kozi ya awali inayotarajiwa kumalizika hapo kesho walitarajia kuwa na washiriki 50 suala ambalo limekuwa vigumu kuweza kuwapata washiriki wengi hivyo wanatarajia kuendelea kutoa kozi hiyo kila mara ili kuweza kufikia idadi ya waamuzi watakaoweza kutosha katika ligi za mchezo huo.

Mkarambati amesema, mashindano ya mashule pia yamechangia kuweza kutafuta waamuzi hao kwani ni shule nyingi zinazoshiriki mchezo hiuo, hivyo waamuzi wamekuwa ni wachache suala linalopelekea mchezo huo kushindwa kusambaa katika shule zote.

Mkarambati amesema, kozi hiyo haichukui walimu peke yake bali inachukua wachezaji wenye uelewa na kazi ya uamuzi ambao watapewa mafunzo ya jinsi ya kuusimamia mchezo huo.