Wachezaji Mbeya wakishangilia bao katika mechi yao dhidi ya Yanga
Kocha Phiri alisema kuwa nguvu kubwa ya ushangiliaji iliyokuwa inatoka upande wa jukwaa la mashabiki wa City iliwafanya wachezaji kutambua kuwa wanalo jukumu kubwa la kucheza kwa nguvu na umakini mkubwa kuhakikisha wanapata matokeo ambayo yangekuwa faraja pekee kwa mashabiki wao waliojitokeza uwanjani kwa wingi.
“Hakika ilikuwa siku nzuri, mashabiki walijitokeza kwa wingi, nguvu yao ya ushangiliaji ilishtua mioyo ya wachezaji wangu wakatambua kuwa wana deni kubwa la kusherehesha furaha kwa mashabiki wao kwa kufanya jambo moja tu la kucheza kwa nguvu na umakini kuhakikisha wanashinda na kupata pointi tatu kutoka moyoni ninawashukuru sana walifanya kazi kubwa” alisema Phiri.
Kinnah Phiri - Kocha Mbeya City
Kuhusu hali ya kikosi na mpango wa kushinda mchezo huo kiufundi, Kocha Phiri alisema kuwa, awali aligundua nguvu kubwa ya Yanga inatoka pembeni ya uwanja huku akianikizwa na viungo wa katikati hivyo alilazimika kubadili mfumo na kikosi kuhakikisha timu hiyo ya Dar es Salaam haipati mwanya wa kupita au kutengeneza nafasi ya kufunga bao.
“Yes! nilifanya maamuzi mengi tofauti hii ni baada ya kuifuatilia Yanga kwenye michezo kadhaa, nilibadilisha kikosi nikabadilisha mfumo, Yanga ni timu nzuri huwezi kuiweka kwenye kundi la timu ndogo lakini ubora wetu kwenye mchezo wa jana uliwanyima nafasi ya kucheza mchezo wao waliouzoea na kushindwa kuleta hatari langoni kwetu, vijana wangu walicheza kwa namna nilivyowaelekeza ndiyo sababu kila mmoja aliona tumecheza vizuri ” alisema Phiri.