Monday , 27th Oct , 2014

Matokeo ya sare Tano mfululizo kwa magwiji wa soka hapa nchini wekundu wa msimbazi Simba yamewashitua viongozi wa timu hiyo na kuanza kuchukua hatua za haraka huku wakiendelea na uchunguzi wa kina juu ya tatizo ama kiini cha matokeo hayo ya sare

Kikosi cha timu ya soka ya Simba katika picha ya moja ya michezo ya ligi kuu Tanzania bara.

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umewarejesha jijini Dar es salaam wachezaji nyota watatu wa timu hiyo ambao wamesimamishwa kwa sababu tofauti.

Wachezaji waliosimamishwa ni pamoja na kiungo galacha Amri Kiemba na Haruna Chanongo ambao wanatuhumiwa kucheza chini ya kiwango katika michezo kadhaa ambayo timu hiyo imecheza na yote kuambulia sare.

Mchezaji mwingine ni kiungo fundi Shaban Kisiga 'Malone' ambaye amesimamishwa kwa utovu wa nidhamu mara baada ya kutofautiana na viongozi wake walioambatana na timu hiyo jijini Mbeya ambako timu hiyo ilicheza na maafande wa Tanzania Prisons nakutoka sare ya bao 1-1.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba Zakaria Hans Pope amesema maamuzi hayo ni moja ya hatua za awali za kuinusuru timu hiyo katika mwenendo huo mbovu ambapo mpaka sasa timu hiyo imecheza michezo mitano na kutoka sare yote

Aidha Hans Pope amesema wataangalia matokeo ya mchezo ujao hasa katika suala la wachezaji kucheza kwa kujituma na kuonesha uwezo wao na kama hali ya kutofanya vema itaendelea kuwepo basi wataangalia pia kwa upande wa pili wa benchi la ufundi ikiwemo kuangalia mbinu za kocha mzambia Patrick Phiri na wasaidizi wake au pia pengine wachezaji hao waliosimamishwa wanakuwa hawapangwi katika namba walizozizoea kitu ambacho kinawafanya kutoonesha uwezo wao na kufanya ufanisi wa timu kupungua na hivyo kufanya timu kupata matokeo ya sare kila mchezo

Hans Pope ameongeza kusema kuwa anashangazwa na kikosi cha timu hiyo kupata matokeo hayo wakati timu inawachezaji nyota wengi na wanaowika katika timu zao za taifa na pia uongozi wa timu hiyo uko vizuri kila idara na hakuna matatizo yoyote ya kambi wala madai ya posho au hata malimbikizo ya mishahara kwa wachezaji

Pia Pope amesema 'labda matokeo hayo yanatokana na kutoelewana kitimu kutokana na wachezaji wengi wapya lakini hali hiyo isitafsiriwe kama kuna kundi la watu fulani [Simba Ukawa] kama ndio wanasababisha matokeo hayo kitu ambacho si cha kweli

Timu ya Simba iko mjini Makambako ambako itaweka kambi kwa siku chache kabla ya kuelekea Morogoro ambako itakuwa na kibarua pevu tena kizito mno itakapovaana na vinara wa Ligi Kuu Tanzania bara timu ya Mtibwa Sugar mchezo utakaoipigwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Wakiwa mkoani Iringa wanamsimbazi hao ambao jana walikuwa katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine kuwashuhudia Mtibwa wakiwaduwaza Mbeya City kwa mabao 2-0 wanataraji kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya daraja la kwanza Tanzania bara FDL Lipuli FC ya Iringa mchezo utakaopigwa katika dimba la kumbukumbu ya Samora.