Friday , 8th Dec , 2017

Baada ya timu ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars kupoteza mchezo dhidi ya Zanzibar Heroes  kwenye michuano ya CECAFA Senior Challenge hapo jana kocha mkuu Ammy Ninje amesema bado timu hiyo ina nafasi ya kufanya vizuri.

Ninje amesema makosa mawili yaliyofanywa na wachezaji wake ndio yaliwaghalimu kwenye mchezo wa jana lakini hawapaswi kulaumiana kwani bado wanayo nafasi ya kufanya vizuri kwenye michezo iliyobaki na kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayoendelea nchini Kenya.

“Kuliko kuangalia makosa ya mchezaji mmoja mmoja nimewaambia wachezaji wangu wasikate tamaa bado tuna nafasi ya kufanya vizuri katika mechi zetu mbili zilizobaki,” amesema Ninje.

Kilimanjaro Stars iliyopo katika kundi A imebaki na michezo dhidi ya Rwanda na wenyeji Kenya ambayo Kocha Ninje anaamini watashinda na kusogea hatua ya nusu fainali ya michano hiyo iliyoanza Disemba 3 ikitarajiwa kumalizika Disemba 17.

Kwa matokeo hayo Kilimanjaro Stars inabakiwa na pointi 1 baada ya kucheza michezo miwili katika kundi hilo la A ambalo linaongozwa na Zanzibar Heroes yenye alama 6 baada ya michezo miwili.