Monday , 4th Jan , 2016

Kibarua cha kocha wa klabu ya Real Madrid Rafael Benitez kipo mashakani kufuatia bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo kufanya mkutano mchana wa hii leo baada ya mechi ya jana dhidi ya Valencia iliyomalizika kwa sare ya bao 2-2.

Kocha mkuu wa Real Madrid ambaye kibarua chake kipo mashakani Rafael Benitez akiwa anawasili klabuni hapo mwaka jana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na radio moja nchini Hispania imesema kuwa bodi hiyo ikiongozwa na Rais wa klabu Florentino Perez imeketi na huenda wakafikia maamuzi magumu ya kumtimua kocha huyo huku nafasi yake ikitarajiwa kutwaliwa na Zinedine Zidane.

Benitez aliyetua klabuni hapo akitokea Napoli ya Italia amekuwa kwenye wakati mgumu mwezi uliopita kutokana na timu kuonekana kucheza chini ya kiwango huku ikiripotiwa kuwa na mahusiano mabovu na baadhi ya wachezaji.

Mpaka sasa Real Madrid inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga kwa point 37 pointi mbili nyuma ya Barcelona walio katika nafasi ya pili huku Atletico Madrid wakishika nafasi ya tatu kwa point zao 42.