Akizungumza na East Africa Radio, makamu mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu nchini TAVA, Muharame Mchume amesema, michuano hiyo iliyoanza jana ilishirikisha nchi saba ambazo ziligawanywa katika makundi.
Mchume amesema makundi hayo yalikuwa mawili ambapo Tanzania ambayo ni nchi wenyeji katika michuano hiyo ilikutana na Kenya na Misri ambapo Tanzania ilitolewa katika michuano hiyo huku kundi la pili likiwa na nchi za Rwanda, Burundi, Eritrea na Uganda ambapo Eritrea na Uganda zilizolewa katika michuano hiyo.
Mchume amesema, Tanzania ambayo ni nchi wenyeji wa michuano hiyo, ilitolewa katika hatua ya awali na hiyo ilitokana na kuwa na uzoefu mdogo lakini mpira ni kama sayansi ambapo unaweza ukafungwa ugenini au nyumbani suala linalotegemea na maandalizi.
Kwa upande wa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Nassoro Sharrif amesema, Timu yake imetolewa kutokana na uzoefu na hata timu walizoshindana nazo zilikuwa na maandalizi ya muda mrefu ambayo ni mipango mikakati ya miaka mingi ya kuziandaa na kuzikuza timu hizo.
Shariff amesema, kwa upande wa Tanzania kuna mipango ambayo inaendelea ikiwa ni sehemu ya kukuza mchezo huo yamesaidia kuwawezesha kufanya vizuri.