Afisa Habari wa TFF Baraka Kizuguto amesema, Kanuni na taratibu za CAF ziko wazi kuhusu nani aongoze ZFA na anapatikana kwa utaratibu upi na kikubwa ni kuzuia ZFA isipate madhara ya kufungiwa na Chama Cha Mpira wa Miguu barani Afrika CAF.
TFF wametoa kauli hiyo baada ya wajumbe wanaounda kamati ya muda ya ZFA kumtaka Rais wa TFF, Jamal Malinzi aombe radhi kabla hawajamfikisha mahakamani baada ya wiki iliyopita kutoa tamko la kutoitambua Kamati ya Muda ya ZFA na badala yake wanamtambua Rais wa ZFA, Ravia Idarous Faina.
Makamu wa Rais wa ZFA, Haji Ameir Haji alisema wamesikitishwa na kauli ya Malinzi aliyoiita 'potofu' huku akidai kuwa kamati hiyo ilichaguliwa kihalali na inatekeleza yale yaliyoagizwa na sasa soka la Zanzibar linaendelea kama walivyokubaliana.
Haji alidai kuwa ZFA wanamuona Malinzi ndiye chanzo cha migogoro yote visiwani humo licha ya kuwa mwenyekiti katika mkutano wa usuluhishi uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukubaliana kamati ya muda iundwe ambayo sasa anadai haitambui.
Haji alisema ZFA wanaitambua TFF na wanajua wako pamoja, lakini katika baadhi ya mambo, kila chama kinapaswa kufanya kivyake, ili kila nchi ishiriki kivyake katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo kwa vile "kila nchi ina wizara yake ya michezo".
Haji aliongeza kuwa amesikitishwa na kitendo cha Malinzi kuchochea ZFA wafukuzwe uanachama katika Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Alidai kuwa Malinzi anafanya hivyo ili ZFA wapokwe nafasi ya kuandaa mashindano ya Kombe la Kagame ilhali Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limeshaitangaza Zanzibar itakuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka huu.
Kutokana na mambo hayo, kamati hiyo ilimtaka Malinzi aombe radhi kabla hawajamfikisha mahakamani.
Katika mkutano huo, Haji alifuatana na wajumbe watano wa Kamati ya Muda ya ZFA wakiwamo katibu mkuu, Salim Hamdoun Hamed na wajumbe Taifan Vuai Makame, Masoud Atta Masoud na Hashim Salum Hashim.




