Monday , 5th Dec , 2016

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga SC, imekanusha taarifa ya kumsajili mshambuliaji kutoka kwa mahasimu wao Simba SC, Ibrahim Ajibu na kuweka wazi kuwa nyota huyo hayumo kwenye mipango ya Yanga.

Ibrahim Ajibu

Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit amesema kuwa hawana mpango na endapo ingekuwa kila kitu kingekuwa wazi, na wangefuata utaratibu.

"Hatuna matatizo na Simba, Simba ni ndugu zetu, kwahiyo wanaodai kuwa jina la Ajibu limetokea Yanga ni wazushi kwa kuwa hakuna mtu anayeweza kuona usajili wa timu isipokuwa CAF na mtu wa TMS wa TFF" Amesema Baraka.

Kwa upande wao wekundu wa Msimbazi Simba kupitia kwa msemaji wao Haji Manara pia wamesisitiza kuwa taarifa hizo siyo za ukweli kwa kuwa Ajibu bado ni mchezaji wa Simba na anaendelea na mazoezi na klabu hiyo kama kawaida, na kwamba hakuna taarifa zozote za kusajiliwa kwake na timu nyingine.

Haji Manara

"Bado Ajibu ana mkataba na kila siku anakuja na mazoezini, taarifa zinatengenezwa, ili sisi tufanye kazi ya kukanusha, yaani story inapikwa bila kutaja source ni nani, Ajibu hajasema, Yanga haijasema wala sisi hatujasema" Amesema Manara.

Kuhusu mazoezi, Manara amesema klabu hiyo inaingia kambini mkoani kesho ikihusisha wachezaji wote, na Ajibu akiwemo.