Monday , 3rd Nov , 2014

Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA linatarajia kutoa kozi ya makocha na waamuzi kwa upande wa wanawake hapo mwakani ili kuweza kupata makocha wazuri watakaoweza kukuza soka hapa nchini.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Salum Madadi amesema waliomba kozi hiyo ikiwa na lengo la kupata makocha na waamuzi maalum kwa ajili ya kusimamia mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Madadi amesema katika mafunzo hayo kutakuwa na madarasa maalum ya hatua ya awali ya makocha pamoja na hatua ya awali ya waamuzi ambapo anaamini kwa kupitia kozi hizo timu mbalimbali za wanawake zitaweza kuwa na uwezo wa kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa kuwa na makocha wazawa na wenye ujuzi wa soka la kisasa la wanawake.