Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba (kulia) akiwa na mmoja wa makocha waliowasili leo kutoka Hispania, Zebensul Hernandez Rodriguez.
Makocha wawili kutoka klabu ya Deportivo Tenerife ya Hispania wamewasili jioni ya leo kwa ajili ya kuja kufanya mazungumzo ya kusaini Mkataba wa kufundisha Azam FC.
Makocha hao Jonas Garcia Luis na Zebensul Hernandez Rodriguez wamewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jioni hii na kupokewa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba.
Mara baada ya kuwasili JNIA, makocha hao wamesema kwamba wanatarajia kupata mwongozo wote kutoka wenyeji wao na wasingeweza kuzungumza mambo mengi.
Kawemba amesema kwamba wawili hao wamekuja kwa mazungumzo ambayo kama yatakwenda vizuri wataajiriwa kwa ajili ya kufundisha timu kuanzia msimu ujao.
Kawemba amesema kwamba makocha hao watasafiri kwenda Tanga kesho kuiona timu ikicheza na African Sports katika mchezo wa Ligi Kuu kesho Uwanja wa Mkwakwani.
Tayari kocha Muingereza, Stewart John Hall amekwishaaga kwamba ataondoka mwishoni mwa msimu, ambao unakamilika Juni.
Kupatikana kwa makocha hao ni matunda ya winga chipukizi wa Azam FC, Farid Mussa kwenda kwenye majaribio Hispania.
Farid amefuzu majaribio katika klabu ya Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania, na sasa klabu hiyo imeanza majadiliano na Azam FC juu ya biashara ya mchezaji huyo.
Nyuma ya biashara hiyo, Azam na Tenerife wanaelekea kufunga ndoa nzito ambayo matunda yake ni ujio wa makocha hawa watakaofundisha kuanzia timu za vijana.
Makocha hawa wanataka pia kubadilisha kabisa mfumo wa akademi ya Azam FC kwa kuchukua vijana wadogo zaidi kuanzia umri wa chini ya miaka 12.