Monday , 15th Dec , 2014

Timu ya vijana kutoka mkoa wa Dodoma imeendelea kufanya vizuri katika michuano ya Copa Coca-Cola ngazi ya Taifa baada ya kuifunga timu kutoka mkoa wa Katavi Goli 5-3.

Akizungumza na East Africa Radio, Kocha wa Timu ya Mkoa wa Dodoma, Mussa Furutuni amesema nia yao ni kuendelea kufanya vizuri na kuibuka mabingwa katika michuano hiyo na hayo yote hayawezi kufikiwa iwapo hawatajijenga katika mazoezi.

Furutuni amesema zoezi la Shirikisho la Soka nchini TFF, kusimamia suala la umri limeendelea kusaidia kwa kiasi kikubwa katika michuano hiyo kwani timu zote shiriki zimeleta umri sahihi kwa ajili ya michuano hiyo.

Kwa upande wake, Nahodha wa Timu ya Mkoani Dodoma, Davson Meddy amesema japo wanafanya vizuri katika michuano hiyo lakini ushindani ni mkubwa kutokana na kila timu kuhitaji kuibuka na ushindi katika kila mechi ili iweze kuibuka na ushindi wa Michuano hiyo ya Copa Cocacola.

Kwa upande wake Kocha wa Timu ya Katavi, Mohamed Bacho amesema vijana wake wamecheza mechi kwa kuonesha viwango walivyonavyo lakini walishindwa kufanya vizuri na kupoteza mechi zote mbili.

Bacho amesema kushindwa kufanya vizuri kwa wachezaji wake kumesababishwa na uchovu kwani walifika usiku sana na asubuhi walikuwa na mechi huku uzoefu wa uwanja kwa vijana wake nao ukichangia kwani kulikuwa na jua kali suala lililopelekea wachezaji kushindwa kufanya vizuri.