Mashabiki wa Yanga 'wakimgombania' kipa wa timu yao, Deo Munishi 'Dida' wakati timu ilipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Yanga wamerejea nchini na kupokelewa na mashabiki wao waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Ilikuwa furaha kuu, haikuishia hapo, wakaanza safari ya kukatisha mitaa huku mashabiki wakikimbia barabarani.
Mashabiki hao waliandamana kupitia barabara ya Pugu hadi walipofika katika jengo la Quality Plaza.
Mashabiki wengine walikuwa wamepanda juu ya miti na juu ya majengo mbalimbali, lengo likiwa ni kutaka kuwaona Yanga hasa kipa wa timu hiyo Deo Munishi maarufu kama Dida ambaye kila shabiki alimwimba kwa nyimbo za pongezi wakimtaja kama ndiye shujaa wao baada ya kuokoa mkwaju wa penati dakika za mwisho na kuzima kabisa ndoto za Waangola.
Kiukweli hii leo Ilikuwa ni shangwe kubwa kila sehemu wakati Mabingwa hao wa Tanzania, Yanga wakirejea nyumbani baada ya kufanikiwa kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Wachezaji na mashabiki, walionekana kupagawa kwa furaha huku wakitamba kuanzia kwenye viwanja vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, hadi barabarani wakiwasindikiza mashujaa wao.
Yanga ambao tayari ni mabingwa wa ligi kuu bara usiku huu wanaelekea mjini Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya kukamilisha mchezo wa mwisho wa kufunga pazia la ligi kuu Tanzania bara dhidi ya wenyeji wanalizombe Majimaji mchezo utakaopigwa siku ya jumapili Mei 22 mwaka huu katika uwanja wa Majimaji.
Na mara baada ya mchezo huo Yanga ambayo inasubiri kujua ni timu gani na kundi gani atapangiwa katika hatua hiyo ya makundi barani Afrika wanataraji kurejea jijini Dar es Salaam mara tu baada ya mchezo wao dhidi ya Majimaji tayari kwa mchezo wa fainali ya kombe la FA ya TFF dhidi ya Azam fc mchezo utakaopigwa Mei 25 mwaka huu katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.