Philippe Coutinho akishangilia moja ya mabao yake matatu wakati Brazil ikiibuka na ushindi wa 7-1 dhidi ya Haiti
Kiungo wa klabu ya Liverpool ya England, Philippe Coutinho alfajili ya leo alikuwa mwiba mkali kwa walinzi wa timu ya Haiti baada yakufanikiwa kuiwezesha timu yake ya taifa ya Brazil kuibuka na ushindi mnono na wakihistoria akiifungia timu hiyo mabao matatu kati ya 7 wakati timu hiyo ikishinda kwa 7-1.
Pamoja na mabao hayo mazuri ya Coutinho [hat trick] mbele ya Haiti kwenye mchezo wa mashindano maalumu ya Copa America kuazimisha miaka 100 ya michuano hiyo, Brazil ilicheza soka safi na ilipania kuibuka na ushindi tangu dakika za mwanzo za mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Camping World mjini Orlando, Marekani.
Mabao mengine ya Brazil yamefungwa na Renato Augusto aliyefunga mabao mawili, Gabriel Barbosa na Lucas Lima, wakati la Haiti bao lao limefungwa na James Marcelin.
Ushindi huo mujarabu kwa Wabrazil ni kama kufuta machungu ama kujifariji na kipigo cha bao 7-1 walichokipata wao tena katika ardhi ya nyumbani kwao mbele ya Wajerumani mnamo mwaka 2014 katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia.
Na sasa matokeo hayo yanaiacha Brazil inayonolewa na kiungo bora mkabaji wa zamani wa timu hiyo Carlos Dunga wakiwa mbele kwa alama nne zaidi kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya akundi dhidi ya Peru.