Beki wa kulia wa timu ya soka ya Yanga, Juma Abdul.
Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyoketi Jumamosi Iliyopita, imeonesha kwamba Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara VPL msimu wa mwaka 2015/16.
Rekodi hizo pia zinaonyesha kwamba beki huyo hakuonyeshwa kadi hata moja katika michezo hiyo mitano sambamba na kutoa mchango mkubwa katika michezo aliyoshiriki kwa mwezi Aprili, 2016. Abdul atazawadiwa fedha Sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo, Kampuni ya mahiri ya simu za mkononi ya Vodacom.
Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mapharao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.
Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Young Africans (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari 2016) na Shiza Ramadhani Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).